Ticker

6/recent/ticker-posts

MAFANIKIO YA SERIKALI YA AWAMU YA SITA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA DODOMA


Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Dodoma Dkt. Ibenzi Ernest akielezea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kipindi cha miaka miwili madarakani katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa jengo la Mkapa, leo tarehe 14/02/2023.


Waandishi wa Habari wakisikiliza mafanikio ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma yaliyowasilishwa na Dkt. Ibenzi Ernest (hayupo pichani) katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Dodoma jengo la Mkapa. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma imeandaa programu maalumu ya kutangaza mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita kwa taasisi zilizopo Mkoani hapo.

************************

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma imeandaa programu maalumu ya kutangaza mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita kwa taasisi zilizopo Mkoani hapo ambapo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma Dkt. Ibenzi Ernest ameelezea mafanikio yaliyopatikana kwenye Hospitali hiyo katika kipindi cha miaka miwili.

Amesema Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma inajivunia kuwa miongoni mwa Hospitali za Rufaa za Mikoa nchini zenye utoaji wa huduma bora za mifupa.

“Tunajivunia Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uboreshaji alioufanya kupitia Wizara ya Afya kwani imeboresha misingi ya kutoa huduma kwa wagonjwa wetu na tuna mpango wa kufanya huduma za afya ziwe za kitalii zaidi kwani tunataka mikoa mingine iweze kutoa huduma kama zetu. Tunalenga kwenye utoaji wa huduma bora” Ameongeza Dkt. Ibenzi

Kwa upande wa vipimo vya mionzi, Dkt. Ibenzi amesema kuwa Hospitali imeongeza vipimo vya mionzi kutoka viwili hadi kufikia 7, vipimo vya Ex-Ray vitatu kutoka kimoja cha awali pamoja na kipimo cha CT-SCAN kwa sasa kinapatikana hospitalini hapo. Jengo la bima na lile linalotoa huduma ya Mama na Mtoto yameboreshwa kwa kuwekewa huduma zote za mapokezi, vipimo na dawa sehemu moja kwa lengo la kuboresha huduma kwa wagonjwa.

Katika kipindi cha miaka miwili cha Serikali awamu ya sita imefanikisha kupatikana kwa mitungi ya kuzalishia gesi ya Oxygen ambayo imefungwa kwenye vitanda 261 hivyo kwa sasa huduma hiyo inapatikana hapo na hakuna haja ya kumtoa mgonjwa kwenda Hospitali nyingine kwa ajili ya kupata huduma hiyo.

Dkt. Ibenzi amesema Serikali ya awamu ya sita imefanikiwa kujenga miundombinu ambayo imeweza kurahisisha mawasiliano kati ya wagonjwa na watoa huduma wa hospitali hiyo tofauti na kipindi cha nyuma ambacho miundombinu haikuwa rafiki.

“Kwa sasa Hospitali ina muonekano mpya wa jengo la mapokezi kulinganisha na miaka miwili iliyopita pia Hospitali inajivunia ongezeko la vitanda 36 kwa ajili ya wagonjwa mahututi kati ya vitanda 3 vilivyokuwepo hapo awali” Amesema Dkt. Ibenzi

Hospitali ya Rufaa kwa sasa imeongeza watumishi ili kukidhi mahitaji ya kiwango cha wagonjwa wanaopokelewa kulingana na vitengo mbalimbali vyenye uhitaji ikiwemo Madaktari bingwa ambao idadi yao imefikia 23 kulinganisha na mwaka 2020 walipokuwa 5 tu, wauguzi waliobobea katika fani mbalimbali kama madawa, maabara na watoa huduma wa kutosha kulinganisha na kipindi cha nyuma.

Amesema kuwa upatikanaji wa dawa umeimarika Hospitalini hapo katika kipindi hiki tofauti na miaka miwili iliyopita upatikanaji wa dawa ulikua kwa asilimia 50, na sasa changamoto hiyo imepungua na dawa sasa zinapatikana kwa asilimia 98 na endapo mgonjwa atahitaji dawa na ikakosekana Hospitalini hapo, ni jukumu la mhudumu kwenda kuitafuta inapopatikana.

Post a Comment

0 Comments