*************
Na Magrethy Katengu
MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA) imeendelea na mikakati ya kudhibiti ajali barabarani, baada ya kusitisha leseni za usafirishaji abiria kwa Mabasi 22 kwa kipindi cha mwezi mmoja, kuanzia Januari hadi Februari mwaka huu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mamlaka Udhibiti Usafiri wa Ardhini LATRA wa Johansen Kahatano amesema hatua hiyo ya kusitisha leseni hizo ni baada ya Mabasi hayo kuingilia Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) kuharibu vifaa walivyofungiwa kubadilisha mfumo
“LATRA tumechukua hatua ya kusitisha leseni hizo kwa Mabasi hayo 22 baada ya kufuatilia Mifumo yao husika kuchezewa vifaa vyake na kuviharibu vifaa hivyo kwa kubadilisha mifumo ya umeme.”amesema Kahatano
“Kuingilia Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) ni kinyume na Kanuni ya 51 ya Kanuni za Leseni za Usafirishaji (Magari ya Abiria) za mwaka 2020 ni kosa kisheria, Mamlaka imechukua hatua hiyo ya kusitisha Leseni kwa mujibu wa Sheria ya LATRA ya mwaka 2019 na Kanuni zake za mwaka 2020 ili kuwa fundisho Kwa wengine ,” amesema" Kahatano
Hata hivyo, Kahatano ametoa rai kwa Wananchi kuwajibika kutoa taarifa kwa vyombo husika na Mamlaka husika za Usafiri ili kuchukuliwa hatua stahiki kwa Madereva wote wanaoendesha Vyombo vya moto bila kufuata utaratibu kutokana na vyombo hivyo kufungwa vifaa maalum vya kufuatilia mwenendo wake.
Kuhusu usajili wa Madereva wa vyombo vya moto kibiashara, Kahatano amesema hadi sasa LATRA imemsajili Madereva 13,291 ambapo tayari Madereva 904 wamefanya mitihani ya kuthibitishwa na Mamlaka hiyo.
Hata hivyo, amesema LATRA imetoa wito kwa Wamiliki wa Mabasi yanayotoa huduma za kibiashara kuhakikisha Madereva wao wanafika kwenye Ofisi za LATRA, Tanzania Bara ili kusajiliwa na mwisho wa usajili ni Aprili 30, 2023 mwaka huu.
Mkurugenzi wa Udhibiti Usafiri wa Barabara wa Mamlaka hiyo, Johansen Kahatano akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) katika ofisi za Mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam kuhusu hatua walizochukua kusitisha leseni za usafirishaji abiria kwa Mabasi 22 kwa kipindi cha mwezi mmoja, kuanzia Januari hadi Februari mwaka huu baada ya Mabasi hayo kuingilia Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS)
0 Comments