Afisa Ufuatiliaji Mfuko wa Maendeleo ya Jamii - TASAF wilaya ya Bunda Bw. Alex Kumwalu akifafanua jambo wakati akizungumzza na waandishi wa habari katika mtaa wa Tamau kuhusu walengwa hao kutokuwa na wasiwasi wa upatikanaji wahuduma za TASAF katika maeneo watakayohamishiwa.
Baadhi ya wanufaika wa TASAF wakisubiri kupewa utaratibu na maofisa wa TASAF na CRDB namna watakavyofungua akaunti za kupokelea fedha zao.
Mulid Stefano Afisa wa benki ya CRDB Bunda mkoani Mara akiwapa utaratibu wanufaika wa TASAF namna ya kufungua akaunti zao kwa ajili ya kupokea malipo.
Afisa Ufuatiliaji Mfuko wa Maendeleo ya Jamii - TASAF wilaya ya Bunda Bw. Alex Kumwalu akiwafafanulia jambo wanufaika wa TASAF ili kufungua akaunti zao kwa ajili ya kupokea malipo.
...................................................................
Afisa Ufuatiliaji Mfuko wa Maendeleo ya Jamii - TASAF wilaya ya Bunda Bw. Alex Kumwalu amewahakikishia wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini awamu ya tatu kipindi cha pili kuwa licha ya wanufaika hao kukumbana na kadhia ya kuhamishwa katika maeneo hayo kupisha hifadhi ya taifa ya Serengeti kutokuwa na wasiwasi kwani bado wataendelea kunufaika na mfuko huo kutokana na mkakati wa serikali uliowekwa.
"Kutokana na umuhimu wa jambo hili baada ya serikali kulitwaa eneo la kata ya Nyatwari ili kuja kuwa Hifadhi ya Serengeti kuna maagizo yalitoka serikalini kwamba wananchi wote wa eneo hili waweze kuhamishiwa kwenye maeneo mengine ili kuendelea na shughuli zao,"amesema Alex Kumwalu.
Aidha amesema watahakikisha wanaendelea kuwasimamia kwani huko watakakohamishiwa watatafutiwa maeneo mengine yenye huduma za TASAF kwa ajili ya kuendelea kupata fedha katika mpango huo wa TASAF hivyo amewataka walengwa hao kuondoa wasiwasi kwakuwa huduma hiyo itaendelea kama kawaida.
Kuhusu mfumo wa Malipo ya mtandao Alex ameendelea kusema kuwa malengo yao ni kuendelea kuwahamasisha na kuhakikisha walengwa wote wanapokea fedha zao kwa mtandao ili waweze kuzipata kwa wakati na kuondoa changamoto mbalimbali zikiwemo kuibiwa wakati wanapokabidhiwa mkononi.
"Tunaendelea kuwahamasisha walengwa wote waweze kuhamia kwenye malipo kwa njia ya mtandao na benki ndio maana tupo na watu wa CRDB kwa ajili ya kuwafungulia akaunti, ili hata wakihamia sehemu yeyote waweze kupata fedha zao kwa wakati na itakuwa inaingia moja kwa moja kwenye akaunti zao au kwenye simu zao.
Awali wanufaika wa mfuko huo kutoka mtaa wa Tamau walikuwa na maoni mbalimbali huku wakiwa na mkanganyiko kutokana na kutaarifiwa na serikali kuwa wanatakiwa kuyaachia maeneo yao ili kupisha eneo hilo ambalo limetwaliwa na serikali kwa ajili ya hifadhi ya taifa ya Serengeti.
Akitoa maoni yake mmoja wa walengwa wa TASAF Bi. Defrida Silla amemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungamo wa Tanzania Dkt Samia Suluh Hassan kuwasaidia ili kuendelea kupata malipo ya TASAF wakati watakapohamishwa katika maeneo ambayo walikuwa wakikaa awali kabla ya kuhamishwa kwenda maeneo mengine.
"Hii TASAF imetoa maelekezo kwamba tuendelee kuchukua na tuendelee kufanya maboresho ya vikundi vyetu ili wahakiki na wakija wajue tumeweza kufanyia kazi fedha tulizozipata na sasa ila ka sasa wakati tunahamishwa hatujui kama tutaendelea kupokea hizo fedha za TASAF,"amesema Defrida Silla
Kwa upande wake Bi Sophia Odongo mkazi wa Tamau amesema wakati tunapohamishwa hajui kama wataendelea kupata hiyo fedha ya TASAF kwa sababu tukitawanyika katika maeneo mengine sina uhakika endapo utaratibu wa kunipa hii fedha utaendelea kutokana na kuwa huko nitakakoenda nitakuwa kama nimepoteza mawasiliano.
Takriban wakazi 219 wa Kata ya Nyatwari Halmashauri ya Bunda Mji Mkoa wa Mara wamehudumiwa na kunufaika na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii - TASAF katika mpango wake wa kunusuru kaya masikini ili kuweza kujikwamua kiuchumi.
0 Comments