**********************
Na Shamimu Nyaki
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul amesema Serikali imekuwa ikitoa haki sawa ya ushiriki katika michezo kwa makundi yote ikiwemo watu wenye ulemavu.
Mhe. Gekul ameyasema hayo Februari 03, 2023 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mhe. Khadija Shaaban (Viti Maalum) aliyeuliza Serikali ina mkakati gani wa kuinua ushiriki wa watu wenye ulemavu katika michezo ikiwemo mpira wa miguu, wavu na pete.
"Moja ya mikakati ya Serikali katika kuinua ushiriki wa michezo kwa watu wenye ulemavu hususani mpira wa miguu, wavu na pete ni pamoja na kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kushirikisha watu wenye ulemavu katika matukio yote, kusajili Vyama na Vilabu vya michezo kwa watu wenye ulemavu hususani inayoandaliwa na Serikali," ameeleza Mhe. Gekul.
Mhe. Gekul ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuziwezesha timu za Taifa za watu wenye ulemavu zinaposhiriki katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.
Aidha, Mhe. Naibu Waziri Gekul amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau wa michezo imeendelea kuhamasisha ujenzi wa miundombinu ya michezo yenye mazingira rafiki kwa walemavu.
Aidha, amevitaka vyama, mashirikisho na vilabu vya michezo kusajili watu wenye ulemavu na kuwashirikisha katika matukio yote ya michezo.
0 Comments