MLEZI wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kusini Unguja Dkt.Tulia Ackson, akizungumza na viongozi na wanachama wa CCM(hawapo pichani) katika ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi yaliyofanyika katika skuli ya Kizimkazi Dimbani.
BAADHI ya Viongozi na Wanachama walihudhuria mafunzo hayo wakisikiliza nasaha za mgeni rasmi ambaye ni Mlezi wa CCM wa Mkoa wa Kusini Unguja Dkt.Tulia Ackson.
…………………………….
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
MLEZI wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Mkoa wa Kusini Unguja kichama ambaye pia ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Tulia Ackson,amewataka Viongozi na Watendaji wa Chama kufanya tathimini ya maendeleo yaliyofanywa na viongozi waliopita ili wao wabuni mikakati mipoya ya kuimarisha Chama na Jumuiya zake.
Kauli hiyo ameitoa wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi wa ngazi mbalinbali za CCM Wilaya ya Kusini Unguja yaliyofanyika Kizimkazi Dimbani.
Alisema viongozi hao wanatakiwa kufanya kazi kubwa ya kuendeleza mipango imara ya maendeleo ndani ya chama kwa lengo la kuongeza ufanisi wa kiutendaji.
Dkt.Tulia, alieleza kuwa mafunzo hayo ni muhimu katika kuandaa viongozi na makada wenye uwezo wa kufanikisha ushindi wa Chama Cha Mapinduzi katika Uchaguzi Mkuu wa Dola mwaka 2025.
Katika maelezo yake Dkt. Tulia, alifafanua kwamba kwa sasa mazingira ya kisiasa yamebadilika kwani kila jambo linahitaji elimu na uelewa wa kuchanua ya kiuongozi na kiutendaji.
“Wanachama wenzangu Chama Cha Mapinduzi kinatimiza miaka 46 ambayo ni umri wa mtu mzima hivyo tuna mengi ya kujifunza na kujitathimini wapi tumetoka,tulipo na wapi tunaelekea katika kuimarisha Chama na Jumuiya zake”,alisema Dkt.Tulia.
Pamoja na hayo Dkt. Tulia ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, aliwasihi viongozi hao na wanachama kwa ujumla kusema na kueneza mafanikio yanayotekelezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar Dk.Hussein Ali Mwinyi.
Alisema wanachama wa CCM hawatakiwi kuishiwa na hoja za kuwajibu wapinzani wanaobeza mambo mema yanayotekelezwa na Serikali.
Alisisitiza umuhimu wa Wana CCM kuwatembelea makada na waasisi wa Chama kwani viongozi hao wa zamani wana uelewa wa mambo mbalimbali ya kujifunza.
Alisema viongozi hao wanatakiwa kuongeza idadi ya wanachama kwani ndio mtaji wa kisiasa wa CCM katika uandaaji wa mazingira ya ushindi.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa huo Mwaka Mrisho Ali, alisema kuwa mkoa huo upo salama kisiasa na wamejipanga kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa vitendo.
Mapema Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Kusini Kichama Asha Mzee alisema kuwa mafunzo hayo yamehudhuriwa na jumla ya viongozi 196.
0 Comments