NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Mohammed Said Mohammed,akisalimiana na Viongozi wa CCM Mkoa wa Mjini mara baada ya kuwasili kwa lengo la kufungua mafunzo hayo.
BAADHI ya Washiriki wa Mafunzo hayo wakisikiliza maelekezo ya mgeni rasmi(hayupo pichani) ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Mohammed Said Mohammed.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Mohammed Said Mohammed, akizungumza na viongozi hao wa CCM waliopewa mafunzo ya uongozi.
*********************
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Mohammed Said Mohammed (Dimwa), amepiga marufuku tabia ya baadhi ya viongozi wa Chama kubeba mikoba ya Wabunge, Wawakilishi na Madiwani.
Amesema chini ya uongozi wake hatovumilia vitendo vya baadhi ya viongozi na watendaji kutumiwa na wanasiasa hao kwa maslahi binafsi kukigawa Chama Cha Mapinduzi kwani ni kinyume na utaratibu.
Marufuku hiyo ameitoa katika ufunguzi wa mafunzo ya uongozi kwa viongozi wa ngazi za Matawi hadi Jimbo wa Mkoa wa Mjini Kichama.
Dkt.Dimwa, amefafanua kwamba utamaduni wa baadhi ya viongozi na watendaji wa Chama kutumiwa katika mambo yasiyofaa na wanasiasa hao kunasababisha mipasuko,makundi na utendaji hafifu wa shughuli za taasisi.
Pamoja na hayo amewataka viongozi wa CCM walioomba wananchi ridhaa ya kuwania nafasi za uongozi kuhakikisha wanafanya ziara za mara kwa mara katika maeneo yao kwa lengo la kuratibu na kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo yao.
“ Haiwezekani kiongozi umepewa nafasi ya kuwawakilisha wananchi katika vyombo vya maamuzi ‘Bungeni’ au Baraza la Wawakilishi hufanyi ziara na huendi jimboni na wananchi wako hawana maji,barabara na n.k, nasema nikimbaini kiongozi wa aina hiyo nampeleka Kamati ya Maadili ashughulikiwe”., alisisitiza Naibu Katibu Mkuu huyo.
Akizungumza na viongozi hao Naibu Katibu Mkuu huyo, aliwambia kuwa kiongozi yeyote wa Chama na Jumuiya zake kuanzia ngazi ya Tawi hadi Taifa atakayedharauliwa na Mtumishi wa Serikali na ukapatikana ushahidi usio na shaka mtumishi huyo atachukuliwa hatua za kinidhamu.
Katika maelezo yake Dkt.Dimwa, aliwasisitiza viongozi,watendaji na Wanachama kwa ujumla kuendeleza utamaduni wa kuwa na nidhamu kila mtu kuheshimu mwenzake kwa nafasi yake.
“Chama Cha Mapinduzi ni Chama chenye hadhi kubwa hivyo ni lazima mwanachama ama kiongozi yeyote katika nyumba hii aishi kwa nidhamu na heshima inayoendana na taasisi yetu.”, alisema Dkt.Dimwa.
Kupitia ufunguzi huo wa mafunzo alivitaja vipaumbe vitano (5) atakavyovifanyia kazi kuwa ni pamoja na kufanya kazi kwa kasi na viwango(Speed and standard), kwa lengo la kufikia kwa vitendo dhamira ya maendeleo endelevu ndani ya Chama.
Kipaumbele cha pili alisema ni siasa na uchumi, ambapo aliwasihi viongozi hao kubuni miradi mbalimbali ya kimaendeleo Chama kujiimarisha kiuchumi na kupata fedha zitakazosaidia kuwalipa posho baadhi ya viongozi wa ngazi za chini.
Pamoja na hayo alikitaja kipaumbele kingine kuwa ni pamoja na suala la elimu, kwa kueleza kuwa viongozi wengi wa CCM hawana uelewa katika masuala mbali mbali hivyo wanakiwa kujengewa uwezo wa kitaaluma.
Kipaumbele cha tano alisema ni kuwajengea uwezo wanawake nchini ili wapate uwezo wa kugombea majimbo kwani wamekuwa wakipambana na changamoto nyingi zikiwemo rushwa ya fedha,kutishwa na kukatishwa tamaa.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini Ndg. Talib Ali Talib, alisema dhamira ya mafunzo hayo ni kuhakikisha viongozi hao wanajengewa uwezo wa kiutendaji katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mapema Katibu wa CCM wa Mkoa huo Ndg.Salum Suleiman Tate, alisema kuwa viongozi hao wametoka katika majimbo 9 yenye wadi 18 za Chama cha Mapinduzi wanaoandaliwa kufanikisha ushindi wa CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
0 Comments