Mkuu wa Wilaya ya Bahi Godwin Gondwe akuzungumza wakati alipotembelea Chuo cha VETA Bahi kuangalia hatua xa ujenzi ulipofikia
Mkuu wa Wilaya ya Bahi Godwin Gondwe akipewa maelezo ya Ujenzi wa Chuo cha VETA kutoka kwa Mkuu wa Chuo cha VETA Mkoa wa Dodoma Stanslaus Ntibara wakati Mkuu wa Wilaya alipotembelea chuo hicho.
Baadhi ya Samani zilizo katika Chuo cha VETA Bahi zitazotumika baada ya Chuo kufunguliwa
Baadhi ya Picha za Mkuu wa Wilaya ya Bahi Godwin Gondwe akikagua ujenzi wa Chuo cha VETA Bahi
***************************
Na Mwandishi Wetu , Bahi
MKUU wa Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma Godwin Gondwe ametembelea na kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Bahi .
Akizungumza kwenye ziara iliyofanyika Februari 15 , 2023, Gondwe amesema uwepo wa chuo hicho utaleta chachu ya mabadiliko ya kiuchumi wilayani hapo kwani wananchi watapata ujuzi utakaoongeza thamani katika shughuli zao na kuongeza mapato.
“Tunaamini kabisa ujuzi utakaotolewa hapa utawasaidia wanaBahi kuongeza uzalishaji katika shughuli za kilimo, ufugaji na nyingine na hivyo kuleta tija zaidi,”amesema Gondwe huku akiishauri VETA kuandaa programu za mafunzo kwa kuzingatia zaidi shughuli za kiuchumi za wananchi wa Wilaya hiyo ambazo ni ufugaji, kilimo na madini.
Aidha Gondwe ameitaka VETA kutoa kipaumbele kwenye michezo kwa kutenga maeneo ya wanafunzi kufanya michezo mbalimbali ili kukuza umoja, mshikamano na vipaji wa vijana.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mkuu wa Chuo cha VETA Dodoma Stanslaus Ntibara amesema ujenzi wa chuo hicho umefikia asilimia 90.
Chuo cha VETA cha Wilaya ya Bahi ni miongoni mwa vyuo vipya 25 vya Wilaya nchini ambapo chuo hicho kinajengwa na kusimamiwa na chuo cha VETA Dodoma kwa kutumia nguvu za ndani (Force Account).
Ntibara ametaja kozi zitakazotolewa katika chuo hicho kwa awamu ya kwanza kuwa ni Uhazili na Kompyuta,Ushonaji, Uashi,Ufundi Umeme,Ufundi Magari na Uchomeleaji Vyuma.
Chuo hicho kitakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 300 kwa kozi za muda mrefu na 400 kwa kozi za muda mfupi ambapo nafasi za bweni ni kwa wanafunzi 144.
0 Comments