Ticker

6/recent/ticker-posts

CHUO CHA MIPANGO CHA PONGEZWA KWA SULUHISHO LA CHANGAMOTO YA VYANZO VYA MAPATO KATIKA HALMASHAURI NCHINI.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Prof. Riziki Shemdoe akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa mafunzo elekezi ya kuwajengea uwezo Maafisa Mipango wa Halmashauri na Sekretarieti za Mikoa.

************************

Na SHEILA KATIKULA , MOROGORO

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Prof. Riziki Shemdoe amekipongeza Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) kwa kuibuka na mbinu mbadala ya upatikanaji wa vyanzo vya mapato katika Halmashauri na Sekretarieti za Mikoa Nchi.

Hayo ameyasema jana kwenye hafla ya ufunguzi wa mafunzo elekezi ya kuwajengea uwezo Maafisa Mipango wa Halmashauri na Sekretarieti za Mikoa hapa nchini juu ya Uandishi wa Miradi ya Kibiashara na uanzishaji wa Makampuni (SPV).

“Nimefurahishwa kuona kupitia tafiti mmekuja na suluhisho la uhaba wa vyanzo vya mapato kwenye Halmashauri na Sekretarieti za Mikoa na hivyo kuandaa mafunzo elekezi ya namna Halmashauri zetu na Sekretarieti za Mikoa zinavyo weza kuongeza mapato.

Niwapongeze sana wote mlioandaa mafunzo haya kwa wataalamu wetu ambayo nategemea yatakuja na matokeo chanya”, amesema Prof. Shemdoe.

Prof Shemdoe amezitaka Halmashauri zote nchini kuacha kutegemea mazao ya chakula katika ukusanyaji wa mapato badala yake wabuni vyanzo vingine vitakavyo kuwa endelevu.

"Kutumia vizuizi vya barabarani na kutoza kodi mazao ya chakula ni ishara ya kuishiwa mbinu za ukusanyaji wa mapato.

"Acheni kuwasumbua wananchi, badala yake njooni na vyanzo mbadala na endelevu vya ukusanyaji wa mapato visivyoleta kero", amesema Prof Shemdoe.

Akishiriki hafla ya ufunguzi wa mafunzo hayo kwa njia ya mtandao Makamu Mkuu wa Chuo - Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi wa Chuo cha Mipango Prof, Provident Dimoso ameishukuru Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa namna inavyotoa ushirikiano kwa Chuo cha Mipango katika dhima yake ya kutoa huduma kwa jamii.

Aidha ametoa shukrani kwa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa ufadhili wa utafiti na mafunzo hayo na kuahidi kuwa Chuo kitaendelea kufanya kazi kwa weledi ili kutoa huduma inayojibu changamoto za kimaendeleo zinazoikabili jamii.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa Mwanza Prof,Juvenal Nkonoki akitoa hotuba ya kumkaribisha mgeni rasmi kwa niaba ya Mkuu wa Chuo Prof. Hozen Mayaya alitoa ombi la mafunzo hayo elekezi kufanyika kwa Wenyeviti na Mameya pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini ambapo ombi hili lilikubaliwa na serikali.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki, Jachinda Chang’a amemshukuru Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kutenga muda na kuungana nao katika hafla ya ufunguzi.

"Uwepo wako ni ushahidi tosha kuwa Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan ilivyo na dhamira thabiti ya kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.

Mafunzo hayo yaliyoanza Januari 25 , mwaka huu yameshirikisha Maafisa Mipango kutoka Halmashauri 13 na Sekretarieti za Mikoa 12 ya Tanzania yanayofanyika katika Manispaa ya Morogoro na yanatarajiwa kufungwa Februari 3 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Miko na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Angellah Kairuki.

Post a Comment

0 Comments