Kaimu Meneja wa mradi wa ujenzi wa daraja la mto Mkomazi, Mhandisi Andrew Gewe akiongea na waandishi wa habari.
Daraja dogo lililojengwa na TARURA kwa ajili ya kusaidia wananchi kuvuka katika shuhuli zao za kimaendeleo.
Ujenzi wa daraja la mto Mkomazi ukiendelea eneo la Kwasunga.
********************
Na Hamida Kamchalla, KOROGWE.
WANANCHI zaidi ya 18 elfu wanaotumia daraja la mto Mkomazi, katika Wilaya ya Korogwe wanatarajiwa kunufaika na mradi wa ujenzi wa daraja hilo ifikapo octoba 3, mwaka huu.
Wananchi hao kutoka katika pande mbili ambao wanaunganishwa na mto huo katika barabara ya Kwasunga hadi Mswaha walieleza kwamba kwa miaka mingi wamekuwa wakipoteza ndugu zao kwa kuliwa na mamba pamoja na viboko kuwavamia wakati wa kuvuka kwa kukosa kivuko cha uhakika.
Wakizungumza katika eneo la ujenzi wananchi hao wamesema wanaishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kusikia kilio chao na kuwaletea ujenzi wa daraja hilo kwani wanaamini watakuwa na amani kwakuwa hawataweza tena kuvuka kwa mashaka kwa kuhofia kupoteza maisha kutokana na tishio la mamba na viboko.
"Kabla ya kuletewa ujenzi huu tuliweka daraja la miti lakini tulipokuwa tunavuka kwa miguu mamba walitushambulia na kuua watu, wakati mwengine tulipovushwa kwa ngalawa viboko walitushambulia wanashika upondo na kutuangushia kwenye maji wakati huo mamba nao wanakula watu" amesema Mwajuma Shemhilu, mkazi wa Mswaha.
"Watoto wetu walipokuwa wakienda shuleni mamba waliwakamata na kuwashambulia, tunamshkuru Rais wetu kwa kutuletea ujenzi huu wa daraja watatuweka katika hali nzuri wakati wa kuvuka, Mungu aendelee kumlinda na sisi tunamuombea" ameongeza.
Naye mwenyekiti wa kijiji cha Kwasunga mpirani Lucas Sempoli amesema mto huo unaunganisha kata tatu za Magila gereza, Makuyuni na Mswaha darajani na shuhuli za wananchi ni za ushirikiano kwa pande zote na shida kubwa inatokea wakati maji yanapojaa kwenye mto kwani huleta hatari zaidi ya watu kuliwa na mamba.
"Kuna wanafunzi ambao wanapata huduma ya shule ng'ambo ya huu mto, nao una desturi ya kujaa na iukauka, unapokauka watoto wanapata vizuri lakini ukijaa inakuwa ni hatari zaidi, lakini kwa wananchi, huku ng'ambo kuna mashamba yetu ya asili yako maeneo yote na wananchi wa kata zote tatu tunashirikiana katika mipaka" amesema.
"Kwahiyo watu wa Mswaha majengo anashindwa kuja kwenye mashamba yake huku na mtu wa Kwasunga au Magila gereza wanashindwa kwenda kule kutokana na adha ya maji kujaa kwa kuhofia kuliwa na mamba" amebainisha.
Aidha mwenyekiti amebainisha kwamba hapo awali palikuwa na kivuko wanachovukia lakini mwaka 2009 kilisombwa na maji baada ya mvua nyingi kuonyesha na maji kujaa sana ndipo wananchi wakaamua kujenga kivuko na pia haikusaidia na watu waliendelea kuliwa na mamba.
"Tuliendelea na kilio chetu hiki mpaka Rais wetu Samia Sulluhu Hassan alipotusikia na kuamua kutenga fungus na kutuletea ujenzi wa hili daraja, mradi huu sisi tumeupokea na tunaishukuru hawa wenzetu wanafanya kazi nzuri,
"Na mimi nipo karibu hapa tunashirikiana, kwasababu daraja hili litakapokamilika litaunganisha wananchi wa Wilaya mbili za Korogwe na Handeni, na mbali na hayo hapo katikati Kuna mashamba ya mkonge,
"Ambayo tunategemea wakati wa mavuno Mkonge uchakatwe huko upitishwe hapa uende lakini wakati huu mikonge yetu inaharibika watu wanashindwa kuvuka" amseema.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa mradi huo Mhandisi Andrew Gewe amesema mradi huo umegarimu kiasi cha zaidi ya sh bilioni 3.83, unafadhiliwa na serikali kupitia fedha ya tozo za mafuta na unaendeahwa na Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA) ambao ulianza octoba 3, 2022 na unatarajiwa kumalizika September 9 mwaka huu.
Mhandisi Gewe amesema "mpaka sasa mradi umefikia asilimia 67 na muda ambao umekwishapita ni miezi 9 ambayo ni sawa na asilimia 53 na unaendelea vizuri na tunategemea utakamilika kwa wakati wake".
Hata hivyo Gewe amebainisha kwamba kwa kuona umuhimu wa upatikanaji wa huduma kwa wananchi wameona ni vema kuwajengea kivuko kidogo kwa akili ya watembea kwa miguu tuu.
"Kama mnavyoona maji ya mto huu hayakauki na wananchi wa vijiji hivi walikuwa wanapata tabu katika kuvuka wakitumia mitumbwi, lakini TARURA wakafanya utaratibu wa kujenga daraja kwa ajili ya wananchi kupita kwa miguu",
"Lakini serikali ikaona kwamba kuna umuhimu wa kuweka daraja ambalo litaweza kuhudumia wananchi na maendeleo, kwasababu kuna kilimo cha mkonge kinaendelea pamoja na shuhuli nyingine za kimaendeleo, hivyo serikali ilitenga fedha kwa ajili ya kujenga daraja hili" amebainisha.
0 Comments