****************
Na Magrethy Katengu
BAADHI ya viongozi wa vyama vya siasa nchini wameshukuru hatua iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan ya kufikia maridhiano na vyama hivyo na kuondoa zuio la mikutano ya hadhara, huku wakishauri jina lake kuandikwa kwa wino wa dhahabu.
Viongozi hao wameahidi kushirikiana naye kwa kila nyanja na kwamba watazingatia maneno ya nasaha waliyopewa.
Jana Rais Samia alikutana na viongozi wa vyama vya siasa wapatao 19 na kuahidi mambo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuruhusu mikutano ya hadhara, mchakato wa katiba kuendelea, akiagiza siasa za kistaarabu na kutaka yeye pamoja na chama kilichoko madarakani kukosolewa.
Akizungumza leo Dar es Salaam katika mkutano na wanahabari, Mwenyekiti wa chama cha CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, amesema tukio la juzi ni la kuhistoria na katika awamu zilizopita za uongozi halijawahi kufanyika kwa kuwa viongozi wa vyama vyote walikutana.
Amepongeza kauli za maridhiano na maboresho mbalimbali zilizotolewa na Rais Samia na kwamba ameondoa zuio la mikutano yahadhara lililowekwa kuanzia mwaka 2016.
“Ametangaza rami kuzindua upya mchakato wa kuelekea upatikanaji wa Katiba Mpya, na hilo halina mashaka ya utekelezwaji wake, haswa ikizingatiwa kuwa nchi itafanya uchaguzi wa serikali za mitaa hapo mwakani 2024 na uchaguzi mkuu mwaka 2025,” amesema Prof. Lipumba.
Amempongeza Rais Samia na kumuunga mkono na kwamba ni hatua iliyoungwa mkono na Watanzania wote.
Mwenyekiti wa ADC, Hamad Rashid amesema tukio hilo ni historia zaidi na kupongezwa hasa pale Rais aliposema kuwa atasimamia katiba, sheria na taratibu mbalimbali na kwamba wako tayari kumpa ushirikiano.
“Rais Samia anatembea kwenye maeneo yake, nasaha zake tutazingatia ikiwa ni pamoja na kufanya siasa za kistaarabu,” amesema.
Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Ali Khatibu, amesema vipo vyama vya siasa ambavyo vimekuwa vikijitenga kushiriki matukio mbalimbali, lakini kwa wito wa Rais jana walijitokeza na kuridhika.
Amesema taratibu zitafanywa na baraza la viongozi wa vyama vya siasa, ili kukutanisha viongozi wote kwa pamoja na kutoa tena tamko la pamoja linalohusu yale yaliyofanywa na Rais Samia, huku wakimpa ushirikiano bila kuangalia itikadi za vyama bali kujali uzalendo.
Makamu Mwenyekiti NCCR, Joseph Selasini amesema kwa ruhusa iliyotolewa na Rais Samia ni yenye kuwagusa walio wazembe kutekeleza majukumu yao kwa wakati.
Katibu Mkuu wa Demokrasia Makini, kutoka Zanzibar, Ameir Hassan Ameir, ameshauri siku ya jana kuwa maalum ya kitaifa na kuadhimishwa kwenye demokrasia na jina la Rais Samia liandikwe kwa wino wa dhahabu kwa kile alichokifanya.
0 Comments