Ticker

6/recent/ticker-posts

UKILETWA DODOMA UMELETWA KUJENGA MAKAO MAKUU YA NCHI


Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akizungumza na Watendaji wa Mkoa wa Dodoma mara baada ya kukamilika kwa hafla ya uapisho kwa Mkuu wa Wilaya ya Chemba Mhe. Gerald Mongella na kuwakarisha Wakuu wa Wilaya Bahi Mhe. Godwin Gondwe na Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Sophia Kizigo. Mkuu wa Mkoa wa Dodoma amewaasa kusimamia viapo vyao.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akikabidhi nyenzo za kazi kwa Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Sophia Kizigo mara baada ya kukamilika kwa hafla ya uapisho na ukaribisho kwa Wakuu wa Wilaya waliohamia katika Mkoa wa Dodoma.


Mkuu wa Wilaya ya Chemba Mhe. Gerald Mongella akila kiapo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma leo tarehe 30/01/2023. Hafla hiyo imefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mkapa, Dodoma.

******************************

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amemuapisha Mkuu wa Wilaya ya Chemba Mhe. Gerald R. Mongella pamoja na kuwapokea Wakuu wa Wilaya wapya wawili waliohamishiwa Mkoa wa Dodoma kwenye hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa jengo la Mkapa zilipo Ofisi za Mkuu wa Mkoa.

Mhe. Senyamule amewaasa Wakuu hao wa Wilaya kuheshimu nafasi waliyopewa na Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwani wameaminika kuitumikia nafasi hiyo. “Nafasi ya Ukuu wa Wilaya ina madaraka na dhamana kubwa sana, ukiyatumia kwa tija yanaleta manufaa ila ukiyatumia vibaya utakwenda kupata matokeo mabaya”

Aidha Mhe. Senyamule amesema kuwa Dodoma ni Makao Makuu ya nchi na nafasi waliyopewa wakuu hao ni kuja kuijenga Makao Makuu.

“Kuja Dodoma ni bahati kwakuwa mnakuwa sehemu ya kujenga Makao Makuu ya nchi. Yeyote aliyekuja hapa, ajue amepata nafasi ya kujenga Makao Makuu kwani viongozi wetu wakuu wana matarajio makubwa na sisi. Mkoa umejipanga kuifanya Makao Makuu kama yalivyo matarajio ya viongozi wetu” Mhe. Senyamule

Vilevile Mhe. Senyamule amegusia changamoto zinazoukabili Mkoa wa Dodoma kwenye sekta ya elimu ikiwemo utoro, ufaulu hafifu, ukosefu wa chakula shuleni na upungufu wa miundombinu ya elimu na kuwaagiza Wakuu hao wapya kwenda kusimamia kikamilifu utatuzi wa changamoto hizo kwa kushirikiana na watendaji na wenyeviti wa Vijiji na Kata.

“Halmashauri zetu zina changamoto kubwa kwa upande wa elimu ambazo tunajitahidi kukabiliana nazo kwa mwaka huu. Kwenye upungufu wa miundombinu, nimetoa maagizo kwa wenyeviti wa Kata na Vijiji kukaa vikao na kukubaliana kujenga maboma mawili kwa kila Kijiji kwa mwaka, nendeni mkasimamie agizo hili” Amesisitiza Mhe. Senyamule

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Fatuma Mganga, amepata fursa ya kutoa neno kwa Wakuu hao wapya wa Wilaya wakati wa hafla hiyo;

“Bahi imejipambanua vizuri kwa elimu, miradi na mambo mengine mengi hivyo tunaamini Mkuu wa Wilaya Mpya atakwenda kuendeleza hayo. Wilaya ya Mpwapwa bado ipo nyuma kwenye uandikishwaji wa wanafunzi wanaoingia kidato cha kwanza mwaka huu hivyo tunategemea utakwenda kuhimiza zaidi. Tunategemea Wilaya iwe na vitendo Zaidi kuliko nadharia” Dkt. Mganga

Katika salamu zao za shukrani, wakuu wa Wilaya ya Chemba na Mpwapwa wameahidi kufanya kazi kwa weledi na uaminifu kama viapo walivyoapa vinavyowataka huku wakitekeleza ilani ya Chama Tawala pia wamesema kuwa dhamana waliyopewa ni deni kwa Mhe. Rais aliyewaamini kwa kuwapa na fasi hizo na wanapaswa kulilipa. Wameahidi kuviishi viapo vyao na kwenda kutekeleza maagizo yote ya Mkuu wa Mkoa huku wakiwa tayari kutumika wakati wowote.

Uapisho huo umekwenda sambamba na kumuaga aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mhe. Mwanahamisi Munkunda aliyehamishiwa katika Wilaya ya Temeke Mkoani Dar es Salaam. Wengine waliokaribishwa ni Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mhe. Godwin Gondwe pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Sophia Kizigo.

Post a Comment

0 Comments