Mkurugenzi wa Sera na Mipango Ofisi ya Rais TAMISEMI John Mihayo Cheyo akizungumza kwenye tathmini ya ukusanyaji mapato katika Halmashauri mkoani Ruvuma. Baadhi ya washiriki kwenye kikao cha tathmini ya ukusanyaji wa mapato kwenye Halmashuri kilichofanyika kwenye ukumbi wa mipango ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.
**********************
MKURUGENZI wa Sera na Mipango Ofisi ya Rais TAMISEMI John Mihayo Cheyo amesema ofisi yake inafanya zoezi la tathimini ya ukusanyaji wa mapato katika Halmashuri zote 184 Tanzania Bara.
Amesema zoezi hilo limeanza Januari 9 mwaka huu na linafanyika kwenye Halmashauri na mikoa yote Tanzania bara na kwamba zoezi hilo linajumuisha wataalam kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI,Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA,Wizara ya Fedha,Ofisi ya Mkoa husika na Halmashauri zake.
Akizungumza katika mahojiano maalum Mkoani Ruvuma,Mkurugenzi huyo wa Sera na Mipango amesema kwa ujumla wakurugenzi wa Halmashauri nchini kote wamefurahia zoezi la tathimini ya ukusanyaji wa mapato na wameshauri liwe zoezi endelevu.
“Zoezi hili la tathimini ya ukusanyaji mapato ambalo linafanyika nchi nzima linaweza kutuongezea mapato mengi kwenye Halmashauri na hatimaye kuzifanya Halmashauri zetu kuanza kujitegemea’’, alisisitiza Cheyo.
Hata hivyo amesema kukamilika kwa zoezi hilo kutawezesha kufanya makisio ya mapato ya uhalisia katika Halmashauri kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024.
Mkurugenzi huyo anawapongeza viongozi wote wa TAMISEMI kuanzia Katibu wa TAMISEMI,Kamishina Mkuu wa TRA na makatibu tawala wa mikoa yote nchini kwa kusimamia kikamilifu zoezi la tathimini ya ukusanyaji mapato.
Kwa upande wake Mchumi Ofisi ya Rais TAMISEMI Flugence Matemele ambaye alikuwa kiongozi wa Timu ya Tathimini ya kusanyaji mapato ya ndani kwenye Halmashauri mkoani Ruvuma,amesema zoezi limekwenda vizuri na wakurugenzi wa Halmashauri wametoa ushirikiano wa kutosha.
Amesema katika tathimini hiyo wamefanikiwa kuchambua chanzo cha mapato kimoja kimoja kwa kila Halmashauri kuanzia vyanzo vikubwa wanavyovigemea ambavyo vimebainika vinachangia mapato kuanzia asilimia 22 hadi 58.
Matemele amesema wakati wanafanya uchambuzi huo wamebaini kuna uwekezekano mkubwa wa vyanzo hivyo vya mapato kukusanya mapato mengi zaidi kama vitasimamiwa kwa nguvu zaidi.
“Wakurugenzi wa Halmashauri na watalaam wao wamethibitisha bado walikuwa wanafanya makisio ya bajeti ya kukusanya vyanzo vya mapato kwa kutumia ozoefu tu,lakini katika tathimini hii tumewasisitiza kutumia takwimu’’,alisema Mchumi wa TAMISEMI.
Hata hivyo ameitaja changamoto ambayo imeonekana kwenye tathimini hiyo kuwa ni wataalam kufanya makisio bila kuzingatia takwimu ambapo wataalam hao wameahidi kuanzia sasa watafanya makisio yenye uhalisia.
Amesema zoezi hilo la tathimini ya kusanyaji mapato limeiungaisha TAMISEMI na Taasisi muhimu kama TRA ili kushirikiana na Halmashauri katika uboreshaji ukusanyaji mapato ya ndani katika Halmashauri zote nchini.
Naye Mchumi Mwandamizi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Henry Kaiwanga amesema katika tathimini ya ukusanyaji mapato walioufanya katika Halmashauri za Mkoa wa Ruvuma wamebaini kuwa vyanzo vikuu vya mapato ni mazao ya kilimo,misitu na madini ambapo wamebaini makusanyo yanayokusanywa ni kiwango kidogo sana kutokana na makadirio ya chini.
Hata hivyo amesema wamebaini changamoto ya tofauti ya takwimu kwenye ukusanyaji mapato kati ya TRA na Halmashauri husika ambapo imebainika Halmashauri ina takwimu zake na TRA ina takwimu zake hali inayochangia makusanyo hafifu.
Amesema kutokana na tathmini hiyo wameshauri maafisa mapato wa TRA na maafisa wa Halmashauri kufanya kazi kwa Pamoja ili Taasisi zote mbili zikusanye mapato zaidi.
Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Jumanne Mwankoo ameipongeza Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kufanya zoezi hilo ambalo limekuwa na umuhimu mkubwa katika kuboresha mapato ya ndani katika Halmashauri zote nchini.
Amesema zoezi hilo limeongeza uelewa kuhusu makisio ya mapato ya ndani kwenye Halmashauri kwa sababu wataalam walikuwa wanafanya makisio kwa mazoea.
Hata hivyo uchumi wa Mkoa wa Ruvuma umeendelea kuimarika kwa kuchangia asilimia 3.8 ya pato la Taifa ukiwa juu ya mikoa mingine ya Kanda ya Kusini Mashariki.
Kwa mujibu wa Takwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu,Pato la Taifa (GDP) la Mkoa wa Ruvuma liliendelea kuongezeka kutoka shilingi bilioni 3.147 mwaka 2014 hadi kufikia shilingi bilioni 6.106 mwaka 2021.
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
Januari 15,2023
0 Comments