akiongea jambo na Katibu wa Ccm Mkoa wa Tanga Suleiman Mzee Charasi wakiwa katika mtambo wa kusafisha maji Mowe Jjini Tanga baada ya kutembelea eneo hilo na kujionea hali ya maji ambayo hayakuwa katika hali ya kawaida kwa kuonekana kuwa yamechafuliwa kufuatia shughuli za kibinadamu.
Waziri akikangalia sehemu ya kusafisha maji katika mtambo wa Mowe Jijini Tanga wakati akitembelea eneo hilo na kujionea hali ya maji ambayo hayakuwa katika hali ya kawaida kwa kuonekana kuwa yamechafuliwa kufuatia shughuli za kibinadamu.
Waziri wa Maji Jumaa Aweso akisikiliza kero za wananchi kuhusu ukosefu wa maji jijini Tanga wakati akitembelea katika chanzo cha maji cha bwawa la Mabayani pamoja na mtambo wa kusafisha maji uliopo Mowe na kujionea hali ya maji ambayo hayakuwa katika hali ya kawaida kwa kuonekana kuwa yamechafuliwa kufuatia shughuli za kibinadamu.
**************
Na Hamida Kamchalla, TANGA.
KUFUATIA hali ya ukosefu wa huduma ya maji safi jijini Tanga kwa muda wa siku kadhaa, Waziri wa Maji Jumaa Aweso amewaomna radhi wananchi jijini humo na kutoa maagizo kwa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira (Tanga UWASA) kusimamia na kutekeleza majukumu yao kuhakikisha tatizo Hilo halijirudii.
Waziri Aweso ametembelea katika chanzo cha maji cha bwawa la Mabayani pamoja na mtambo wa kusafisha maji uliopo Mowe na kujionea hali ya maji ambayo hayakuwa katika hali ya kawaida kwa kuonekana kuwa yamechafuliwa kufuatia shughuli za kibinadamu.
"Baada ya kupata taarifa kwa viongozi jijini hapa, nimefika kutembelea chanzo cha maji, watu wote katika jiji la Tanga hutegemea maji kutoka mto Zigi, na kwa hali niliyoikuta pale Yale maji yamechafuka kutokana na shuhuli za kibinadamu zinazofanyika"
"Lakini moja kwa moja nikaenda kwenye mtambo wa kusafisha maji wa Tanga UWASA, kwasababu jukumu la upatikanaji kwa maji kwa jiji la Tanga ni lao, na siyo maji tu bali maji safi, salama na yenye ubora" amesema.
Aidha ameeleza kuwa wataalamu wa mtambo wa kusafisha maji wametoa maelezo kwamba wakiona maji yanayokwenda yamebadilika hivyo kuamua kuzima mitambo kwa muda hali iliyopelekea ukosefu wa maji kwa wananchi.
"Kwahiyo kukosekana kwa maji ndiyo kelele za wananchi zikaanza kuleta taharuki, na ndiyo maana serikali ipo hapa na wale wataalamu wameanza kuyatibu na sasa yako safi na salama, kwa dhati ya moyo kabisa napenda kuwaomba radhi kwa jambo hili lililojitokeza" amesisitiza Aweso.
Hata hivyo Waziri Aweso ametembelea katika baadhi ya nyumba kwenye kata za Chumbageni na Ngamiani kusini na wakati huo baadhi ya nyumba tayari zilishaanza kupata huduma ya maji yakiwa safi na ya kuridhisha.
"Lakini kubwa ninalotaka kulisisitiza, inapotokea tatizo kama hili siyo jambo baya kwasababu utoaji wa huduma ya maji inategemea mitambo, kwahiyo ni wazi wakati mwingine hitilafu zinaweza kutokea, lakini basi utoaji wa taarifa ni lazima ufanyike kwa wakati, kutokutoa huduma bila taarifa lazima kutaleta taharuki" amesema.
"Na ninyi Tanga UWASA, kutoa huduma ya maji siyo hisani bali ni moja ya majukumu mliyopewa na mamlaka yetu, kwahiyo lazima mjipange kutoa huduma wakati wote, mjue mtakacho kufanya iwe jua au mvua watu lazima wapate huduma, maji hayana mbadala" amesema.
Lakini pia Waziri amesema pamoja na huduma hiyo kurejea katika hali yake ya kawaida, "naiagiza Tanga UWASA kuunda timu ya watumishi ambayo itakuwa inapita kila mtaa kuhakikisha watu wanapata maji wakati wote, na mimi macho yangu yatakuwa yanaangalia jiji la Tanga".
Naye Mkurugenzi wa Tanga UWASA Geoffrey Hilly amesema taarifa iliyowafilia wananchi ya kuchafuka kwa maji iliwashtua kwakuwa haikuwa Ile ya kawaida ya kukosekana kwa umeme hivyo kupelekea taharuki na kutaka msaada wa serikali zaidi ndipo Waziri alipoingilia kati suala hilo.
"Tatizo lililotokea ni la kibinadamu na siyo like la shida ya umeme tulilozoea, majanga ya uchafuzi wa maji yametokea kwenye chanzo lakini tunaomba radhi kwa wananchi kufuatia hali hii ya kukosa maji kwa siku kadhaa, tumeshaboresha huduma yetu na kuanzia sasa maji yatarudi katika hali ya kawaida".
0 Comments