Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kituo cha utoaji huduma jumuishi kwa manusura wa ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto kilichopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma. Kituo hicho kimefadhiliwa na Shirika la EGPAF kupitia “mradi wa Afya Yangu”. Uzinduzi huo umeshuhudiwa na Bw. Chip Lyons Rais EGPAF kutoka Marekani.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akiwa katika picha ya pamoja na ugeni kutoka Shirika la EGPAF ukiongozwa na Rais wao Bw. Chip Lyons kutoka Marekani na USAIDS ambao wamesaidia ukarabati wa kituo cha utoaji huduma jumuishi kwa manusura wa ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto kilichopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
………………………
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amezindua kituo cha utoaji huduma jumuishi kwa manusura wa ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto kilichopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Akizindua kituo hicho Mhe. Senyamule amesema Mradi wa USAID Afya Yangu umekuja kwa wakati muafaka kwani Mkoa wa Dodoma ni kati ya Mikoa yenye changamoto za matukio ya ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya Watoto, hivyo kituo hicho cha kwanza katika Mkoa kitasaidia manusura wa ukatili ambao watapata huduma zote kwa haraka kwa wakati muafaka.
“Jengo hili la kutolea huduma jumuishi kwa manusura wa vitendo vya ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto ambalo ninalizindua leo ni moja ya malengo ya mpango jumuishi wa utoaji huduma kwa manusura wa vitendo vya ukatili uliozinduliwa mnamo mwaka 2013. Lengo la kuanzishwa vituo hivi ni kuhakikisha huduma zinatolewa kwa manusura wa vitendo vya ukatili kwa uharaka na kwa uratibu mzuri pia kurahisisha mfumo wa rufaa kwa manusura katika kupata huduma maalum zingine kama vile msaada wa kisheria” Alisisitiza Mhe. Senyamule
Manusura wa vitendo vya ukatili wamekuwa wakipata changamoto katika kupata huduma kwa uharaka na kwa uratibu mzuri kutokana na mtawanyiko wa maeneo ya huduma muhimu wanazozihitaji ikiwemo huduma za afya, Ustawi wa Jamii na huduma za kisheria. Hali hii imesababisha baadhi ya manusura kukosa huduma kwa wakati na kupata madhara yakiwemo maambukizi ya Virusi vya Ukimwi, Ulemavu wa kudumu, mimba zisizotarajiwa na mimba za utotoni zaidi kutokana na vitendo vya ukatili walivyofanyiwa.
“Uwepo wa kituo hiki cha utoaji huduma jumuishi katika Mkoa wa Dodoma utawawezesha manusura wa vitendo vya ukatili kupata huduma kwa uharaka na kwa uratibu mzuri na mwisho kuwawezesha kupata haki zao katika vyombo vya sheria” Amesisitiza Mhe. Senyamule.
Mhe. Senyamule amempongeza Bw. Chip Lyons Rais wa shirika la EGPAF kupitia “mradi wa Afya Yangu” kwa kusaidia ukarabati wa jingo la kituo hicho pamoja na kuwezesha upatikanaji wa vifaa kwa ajili ya kuanza kutoa huduma.
0 Comments