04/01/2023 DODOMA
Jeshi la Polisi nchini limetoa rai kwa wazazi na walezi kuhusu suala la kuimarisha malezi ya familia hususani katika eneo la ukuaji wa watoto ili kuwaepusha kujiingiza kwenye vitendo vya kihalifu pamoja na kuwaepusha kufanyiwa vitendo vya ukatili.
Kauli hiyo imetolewa na Mrakibu wa Polisi SP Dkt. Ezekiel Kyogo kutoka Kamisheni ya Polisi Jamii Dawati la Ushirikishwaji wa Jamii Makao Makuu ya Polisi Dodoma wakati walipotembelea kituo cha kulelela watoto wenye uhitaji mbalimbali kiitwacho Chigongwe Family ambapo jamii imetakiwa kutowatelekeza watu wenye uhitaji na badala yake kuendelea kuwasaidia.
Naye mmoja wa watoto wanaopatiwa malezi kwenye kituo hicho Paul Charles amesema licha ya kutoka kwenye mazingira magumu lakini kwa sasa jamii imejitokeza kuwasaidia kwa kuwapatia hifadhi na mahitaji mengine ya msingi.
Naye Mrakibu Msaidizi wa Polisi ASP Manase Dotto kutoka Dawati la Usalama Wetu Kwanza amesema kuwa, Jeshi la Polisi linaendelea kuwalinda watoto hivyo waendelea kutoa ushirikiano sambamba na kuripoti vitendo vyovyote vya ukatili watakavyofanyiwa ama kukutana navyo.
0 Comments