Ticker

6/recent/ticker-posts

NATANGAZA VITA ENDELEVU NA WANAOKATA MITI HIFADHINI  -RC RUVUMA

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas akizungumza baada ya kuzindua upandaji miti katika shule ya sekondari Ruhuwiko wilayani Mbinga ,hapa pia anamkabidhi Mwenyekiti wa CCM Kata ya Ruhuwiko mti wa kupanda. Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas akimkabidhi mti wa kupanda Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mbinga Mji Mheshimiwa Kelvin Mapunda kwenye uzinduzi wa upandaji miti katika shule.


Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mheshimiwa Aziza Mangosongo akipanda miti katika shule ya sekondari Limbu wilayani Nyasa

********************

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amesema kuanzia sasa anatangaza vita endelevu na watu wote wanaokata miti kwenye misitu na wanaoharibu vyanzo vya maji.

Ametangaza vita hiyo kwa nyakati tofauti wakati anazindua upandaji wa miti shuleni katika wilaya za Mbinga na Nyasa.

RC Thomas amewaagiza wakuu wote wa wilaya, wakurugenzi, maafisa tarafa,kata na vijiji kusimamia sheria mama ya mazingira ili kulinda misitu na vyanzo vya maji.

“Wilaya ya Mbinga inaongoza kwa kuharibu misitu na kuacha milima ikiwa vipara,ninyi kila mahali mnapoona miti mnatembea na shoka na kuteketeza miti,muone aibu mna ugomvi gani na miti’’,alihoji RC Thomas.

Amesisitiza kuwa anaanzisha ugomvi na wakata miti na wanaoharibu vyanzo vya maji kutokana na kufanya shughuli za kibinadamu hadi ndani ya vyanzo vya maji.

Ameongeza kuwa amebaini maeneo mengi yenye hifadhi za misitu zikiwemo hifadhi ambazo zipo chini ya Wakala wa Misitu Tanzania TFS na kwenye vyanzo vya maji na maeneo ya misitu ya vijiji yanavamiwa na kukatwa miti hivyo amewaagiza wadau wote wa mazingira kuyalinda maeneo hayo kikamilifu.

Ameagiza miti yote inayopandwa itunzwe ili iweze kukua na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi yaliyoanza kuleta athari katika baadhi ya maeneo ikiwemo mito na vyanzo vya maji kukauka na kukosa mvua za uhakika.

Amesema upandaji miti na kulinda vyanzo vya maji iwe ni kampeni ya kudumu,ambapo amesisitiza kuwa ameamua kuzindua kampeni ya kupanda miti katika shule ili kujenga tabia ya kupenda kupanda miti kwa watoto kuanzia shule za msingi, sekondari,vyuo vikuu hadi wanapokuwa watu wazima.

Mkuu wa Mkoa amewaagiza TFS kuhakikisha kila shule mkoani Ruvuma inapewa miche ya miti ya kutosha kwa ajili ya kupanda kwenye mazingira yao.

Awali akitoa taarifa ya upandaji miti katika Wilaya ya Mbinga katika kipindi cha mwaka 2022/2023,Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mheshimiwa Aziza Mangosongo amesema wilaya hiyo ina misitu mitano ya hifadhi ambayo ni Namswea, Liwiliktesa, Kigonsera, Amanimakoro na Lupembe.

Mangosongo amesema wilaya hiyo pia ina mashamba ya miti ya kupandwa ambayo ni Mbambi, Ugano, Likopesi, Ndengu,Mpapa,Lubela,Mahenge na Mbuji na kwamba misitu hiyio inasimamiwa na Halmashauri ya Wilaya na Serikali Kuu.

“Uzinduzi wa upandaji miti katika shule,ni kielelezo cha upandaji miti katika wilaya ya Mbinga ambao unaenda sanjari na ugawaji wa miche ya miti kibiashara iliyooteshwa na TFS’’,alisema.

Amesema TFS katika wilaya ya Mbinga imezalisha miche ya aina mbalimbali 208,650 kati yao hiyo misindano 67,120,misaji 9,650,mibolea 13,020, mikaratusi 121,838,miembe 300,michungwa 200, parachichi 500,mikangazi 800 na misedelela 300.

Katika wiki maalum ya upandaji miti mkoani Ruvuma iliyoanzia Januari Mosi hadi 7,2023 jumla ya miche ya miti ya asili 1,100,000 iliyotolewa na TFS imepandwa.

Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma

Januari 13,2023

Post a Comment

0 Comments