Mkuu wa Mkoa wa Tanga Omari Mgumba akizungumza katika kongamano la uzinduzi wa miaka miwili ya uongozi wa Rais Samia Sulluhu Hassan.
Mwenyekiti wa Ccm Mkoa wa Tanga Rajabu Abdalla akiongea katika kongamano hilo.
Wadau mbalimbali wakifuatilia uzinduzi wa kongamano hilo.
*************************
Na Hamida Kamchalla, TANGA.
ZAIDI ya sh bilioni 6.2 fedha za mapato ya ndani ya halmashauri ya jiji la Tanga zimeongezeka ndani ya kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa serikali ya awamu ya sita.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Omari Mgumba alibainisha hayo juzi kwenye uzinduzi wa kongamano la miaka miwili ya uongozi wa Rais Samia Sulluhu Hassan uliofanyika jijini humo ukishirikisha Wilaya zote za Mkoa huo.
"Makusanyo ya mapato ya ndani ya halmashauri yameongezeka kutoka sh bilioni 29.7 mwaka 2020/21 hadi kufikia sh bilioni 35.2 mpaka sasa, hongera sana Mh. Rais Samia Sulluhu Hassan kwa uongozi na maelekezo yako ndivyo vilivyofanya zaidi ya sh bilioni 6.2 zimeongezeka" alisema.
Mgumba alisema kufuatia uongozi uliotukuka Mkoa umepiga hatua kubwa pia katika utekelezaji wa ilani kwa kuweza kukamilisha kwa wakati na kiwango baadhi ya miradi iliyoletewa fedha ikiwa ni pamoja na kuongeza miradi mingine ambayo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
"Ndugu zangu haya ni mafanikio makubwa sana, hakuna sekta ambayo hatujaigusa, kwasababu kuna upotoshaji mkubwa unaendelea huko mitandaoni kwamba hakuna chochote kinachofanyika, lakini ukweli ni kwamba kazi kubwa imefanyika, Rais anaendelea mazuri yote ya wenzake waliomtangulia na kuboresha zaidi" alibainisha.
"Tunafahami kwamba hali ya maisha ni ngumu na hii ni kila mahali duniani, lakini serikali tuna mipango na mikakati, lakini kuna watu wanapotosha kana kwamba hali hii ya maisha na uchumi inaweza kubadilika kwa usiku mmoja" alisisitiza.
Naye Mwenyekiti wa Ccm Mkoa wa Tanga Rajabu Abdalla alisema chama kimeridhishwa na utekelezaji wa ilani uliofanyika mkoani humo na kutoa pongezi kwa viongozi wake kwa kazi nzuri wanaofanya.
Aidha mwenyekiti huyo alisema pamoja na utekelezaji mzuri lakini kuna mapungufu kwa baadhi ya watumishi kwa upande wa sekta ya afya kutoa kauli mbaya kwa wananchi wanaofuata huduma ya matibabu na kusema Ccm mkoani humo haitaweza kumfumbia macho yeyote atakayekwenda kinyume na maadili ya kazi yake.
"Sisi kama wenye ilani, tumeridhishwa na utekelezaji wa ilani, miundombinu ya hospitali ya rufaa ya Bombo imeboreshwa ya kutolea huduma, pamoja na vituo vya afya na zahanati zetu lakini pia watoaji huduma wameongezeka",
"Lakini kwenye mafanikio, kero hazikosekani, katika hospitali zetu kuna kero ya baadhi ya watoa huduma kuwa na kauli mbaya kwa wagonjwa, sisi Chama cha Mapinduzi tunaomba kupaza sauti, na watuelewe ndugu zetu hawa, wasimuharibie Rais wetu, watimize wajibu wao." alisema.
"Inafahamika kuwa, watoa huduma hao wanafanya kazi kubwa katika mazingira magumu ya kuokoa afya za Watanzania wenzao, kwa wale ambao hawataki kubadilika, sisi kama chama tunawaelekeza wabadilike ili waungane na Rais wetu kwenye nia na dhamira nzuri ya kuwatumikia wananchi" alisisitiza.
Pia mwenyekiti alifafanua kwamba katika miaka miwili ya utendaji kazi wa Rais Samia Sulluhu Hassan, Mkoa wa Tanga umepiga hatua kubwa kwa utekelezaji wa ilani katika kila sekta huku miradi mingine ikiendelea kutekelezwa.
0 Comments