Ticker

6/recent/ticker-posts

EFTA KUWEZESHA WAKULIMA ZAIDI YA 200 KUPATA MIKOPO YA MATREKTA BILA DHAMANA

Wakulima nchini wametakiwa kuchangamkia fursa za upatikanaji wa mikopo ya mashine za kilimo inayotolewa bila dhamana na kampuni ya Equity for Tanzania Limited (EFTA), Hatua ambayo imeelezwa kuwa itasaidia katika kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo pamoja na pato la taifa.

Wito huo umetolewa kwa wakulima baada ya kampuni ya EFTA kununua matrekta zaidi ya mia mbili aina ya New Holand TT75 4WD, kwa lengo la kuzikopesha kwa wakulima nchini bila dhamana, hatua ambayo inatajwa kuwa itasaidia kuongeza matumizi ya mashine katika kilimo na hivyo kupelekea Kuongeza kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo, na pato la taifa.

Akizungumzia hatua hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya EFTA bw. Nicomed Bohay amesema kupatikana kwa matrekta hayo mia mbili kutaongeza chachu kwa wakulima katika kuongeza uzalishaji.


“Matumaini yetu ni kuwa kadri wakulima wanavyoweza kumiliki mashine mbalimbali za kilimo ndivyo uzalishaji utakavyoongezeka, Hata hivyo changamoto kubwa ni kuwa wakulima wengi hawakopesheki kutokana na masharti mbalimbali yaliyowekwa na taasisi za kifedha na hivyo kundi kubwa la wakulima kuachwa wakiangaika na kilimo cha jembe la mkono”, amesema.

Baada ya kuiona changamoto hiyo, Bohay anasema ndio maana EFTA kwa kushirikiana na Taasisi zingine kama vile New Holand Agriculture, Hughes Agriculture Tanzania Ltd (HAT) na CRBD Benki wameingia makubaliano yatakayowezesha wakulima nchini kupata mikopo ya matrekta bila dhamana kupitia EFTA hatua ambayo amesema itaongeza idadi ya wakulima nchini watakaoweza kumiliki matrekta bila masharti magumu.


“Kwa wastani kwa Mwaka Matrekta yanayouzwa nchini ni 1800 idadi ambayo bado ni ndogo sana, na katika idadi hii EFTA pekee imetoa matrekta 530 sawa na asilimia 23%. Tamanio leo ni kuona masharti magumu kwa kundi hili tunayaondoa ili idadi ya wakulima wanaotumia mashine bora za kilimo inaongezeka”, amesema Bohay.


Bohay ameongeza kuwa EFTA kupitia makubaliano hayo sasa EFTA itaongeza idadi ya wakulima ambao watakopeshwa matrekta na hivyo kuwa na idadi kubwa ya wakulima wanaotumia matrekta katika kufanya shughuli zao za kilimo.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Plc nchini, Bw. Abdulmajid Nsekela amesema ushirikiano ambao taasisi yake imeuingia na EFTA umelenga kusaidia katika kuwafikia wakulima wadogo nchini kuweza kupata mikopo ya mashine za kilimo kwa masharti nafuu nchi nzima.


"Ushirikiano huu na EFTA umelenga kusaidia wakulima wadogo na wakati nchini kupata mikopo kwa urahisi zaidi bila kuwa na masharti magumu ambayo wakulima wengi hawawezi kuyatimiza”, amesema Nsekela.


“Lengo la Benki yetu ni kuona wakulima nchini wanatumia mashine bora za kilimo maana tunatambua kwa kuwa na wakulima wengi wanaolima kisasa pato la taifa litaongezeka kutokana na uzalishaji utakaofanyika", ameongeza Nsekela.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya New Holand Agriculture Bw. Stuart Leishman, amesema aina ya trekta ambazo kampuni ya EFTA imezinunua ni imara na kuwa zinaweza kufanya kazi katika maeneo yote ya nchi.


“Trekta hizi ni muhimu na zitasaidia kuyafikia malengo ya nchi ya muda mrefu ya kuwa na uhakika wa chakula, na tunajivunia kushiriki katika mchakato wa Kuongeza idadi ya wakulima watakaomiliki trekta na hivyo kuwa na mavuno bora na yaliyoongezeka” amesema Stuart Leishman.


Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Makampuni ya EFAfrica, ambao ndio wamiliki wa Kampuni ya EFTA Bw. Michiel Timmerman amesema amefurahishwa na mpango huu, ambao umelenga kujibu njozi ya kuanzishwa kwa makampuni ya EFAfrica ya kuwasaidia wakulima wadogo na wale wa kati kuweza kumiliki mashine mbalimbali za kilimo bila dhamana hivyo kuchochea ongezeko la matumizi ya mashine katika kilimo.

Post a Comment

0 Comments