Ticker

6/recent/ticker-posts

CCM Z'BAR YAPANIA KUFANYA KAZI NA WADAU WAKE.

KATIBU wa Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Ndg. Khamis Mbeto Khamis, akizungumza kwa mara ya kwanza na watumishi toka ateuliwe kuongoza idara hiyo huko Afisini kwake Kisiwandui Zanzibar.(PICHA NA IS-HAKA OMAR).

**************************

NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

WATUMISHI wa idara ya Itikadi na Uenezi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)Zanzibar wametakiwa kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wabadilike kiutendaji ili watekeleze kwa ufanisi majukumu ya idara hiyo.

Rai hiyo imetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Ndg. Khamis Mbeto Khamis, alipozungumza na watumishi hao kwa mara ya kwanza toka ateuliwe kuhudumu katika nafasi hiyo.

Kupitia mazungumzo hayo yaliyofanyika Afisini kwake huko Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar, Mbeto aliwasihi watumishi hao kuonyesha uwezo wao wa kiutendaji kwa lengo la kuhakikisha wanatimiza malengo ya kulinda,kutetea,kutangaza,kujibu hoja na kueneza sera na muelekeo wa Chama na Serikali zake.

Alisema kuwa anafahamu changamoto zinazowakabili watumishi hao na kuahidi kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu kwa lengo la kuondoa vikwazo vinavyosababisha utendaji usioridhisha.

Alisema Chama Cha Mapinduzi ni lazima kiwaeleze na kuwambia wananchi mafanikio yanayoendelea kupatikana katika utekelezaji na usimamizi wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025.

“ Kwanza nakishukru sana Chama Cha Mapinduzi kwa kuniamini na kikaniteua kutumikia nafasi hii nzito ya kuongoza idara hii ambayo ni mdomo kukisemea Chama na Serikali.

Nasaha zangu watumishi wenzangu tufanye kazi kwa bidii ili Chama kiendelee kuimarika zaidi katika masuala ya kisiasa,kijamii,kiuchumi na kimaendeleo.”, Alisema Mbeto na kusisitiza ushirikiano kutoka kwa watumishi hao.

Akizungumzia vipaumbele vyake alieleza wazi kwamba hatokuwa kiongozi wa kukaa ofisini bali atatembelea na kujenga mahuano na wadau wa Chama hicho ambao ni Vyombo vya Habari,wasanii,wadau katika sekta zote za michezo na wananchi kwa ujumla.

Katika maelezo yake mkuu huyo wa Idara ya uenezi Zanzibar Mbeto, alisema wananchi ndio waoipa CCM ridhaa ya kuongoza dola hivyo wana haki ya kujua taasisi hiyo imesimamia utekelezaji wa ahadi zilizotolewa katika uchaguzi mkuu uliopita kwa kiwango gani.

Aidha alitoa wito kwa viongozi na watendaji wa CCM wa ngazi zote, kuitumia idara hiyo kama kiunganishi cha kutangaza na kueneza masuala ya kisera na kisiasa yanayositahiki kuwambia wananchi kwa mujibu wa Katiba ya CCM.

“Niseme tu kwamba CCM tumejipanga na tupo vizuri kuhakikisha kila mwanachama na wananchi kwa ujumla wananufaika na matunda ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, hivyo kupitia nyenzo zetu rasimi za mitandao ya kijamii tutumieni maoni,ushauri na taarifa za changamoto ili Serikali izitatue.”, alisema Mbeto.

Kipaumbele kingine alisema CCM imejipanga kuimarisha Vyombo vyake vya Habari na kuanzisha vyombo vya habari vingine vitakavyotoa na kueneza kwa wakati taarifa,Itikadi,Sera na miongozo ya Chama.

Katibu huyo Mbeto, aliweka wazi kwamba atasimamia kikamilifu majukumu ya idara kama yalivyoainishwa katika ibara ya 107 cha (2) (a)-(f) ya Katiba ya CCM toleo la mwaka 2022 ya mwaka 1977.

Pamoja na hayo aliwapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kazi kubwa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM pamoja na kuimarisha masuala ya kiuchumi,kisiasa,kijamii na diplomasia za kimataifa.

Awali Mkuu wa idara hiyo alikuwa ni Ndg. Catherine Peter Nao aliyemaliza muda wake wa kuhudumu nafasi hiyo baada ya kuongoza kwa miaka mitano (5), ambapo CCM mnamo Januari 28, mwaka 2023 kupitia Kikao cha Kamati Maalum ya CCM Taifa Zanzibar kimemteua Ndg. Khamis Mbeto Khamis kuwa Mkuu mpya wa Idara hiyo.

Post a Comment

0 Comments