Katibu Tawala Mkoa Mwanza, Elikana Baladya akizungumza kwenye uzinduzi wa Kambi ya madaktari bingwa walipo kwenye hospitali ya Mkoa ya Rufaa ya Sekou Toure iliyopo mkoani Mwanza.
Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Mkoa ya Rufaa ya Sekou Toure,Bahati Msaki akizungumza mara baada ya uzinduzi wa Kambi ya madaktari bingwa walipo kwenye hospitali hiyo.
Wananchi kutoka sehemu mbalimbali wakipewa huduma na madaktari bingwa kwenye kambi ya Sekou Toure iliyopo mkoani Mwanza.
Baadhi ya wananchi kutoka sehemu mbalimbali wakisubili kupewa hudumu kutoka kwa madaktari bingwa.
*************************
Na Sheila Katikula,Mwanza
Wananchi mkoani Mwanza wametakiwa kujitokeza kwa wingi kupima afya zao kwenye kambi ya madaktari bingwa iliyopo katika hospitali ya rufaa ya Sekou Toure.
Hayo yamesemwa leo na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Elikana Balandya kwenye ufunguzi wa kambi ya madaktari bingwa kutoka hospitali ya Kanda ya rufaa Bugando na hospitali ya rufaa Sekou Toure
Balandya amesema hospitali ya Sekou Toure imeendaa kambi hiyo ya madaktari bingwa kwa lengo la kutoa huduma na kuwasaidia wananchi ili waweze kutambua afya zao pamoja na kupata matibabu kwa gharama nafuu.
"Kambi hii ina madaktari bingwa ambao wanatoa huduma mbalimbali kwa wananchi ni vema watu kujitokeza kwa wingi ili muweze kufahamu afya zenu," amesema Balandya.
Amesema huduma zinazotolewa na madaktari hao ni magonjwa ya kina mama na uzazi, Watoto, Macho, Meno, Mionzi, magonjwa ya damu, Mfumo wa chakula, Magonjwa ya akili, Huduma ya kusafisha damu, Huduma za maabara na dawa.
Hata hivyo amesema vipimo mbalimbali vinatolewa vikiwemo Vipimo vya kisukari, vidonda vya tumbo, x-ray, moyo, Figo pamoja na magonjwa ya damu kama vile, selimundu, Kansa ya damu, mchafuko wa damu mwilini.
Kwa upande wake Mganga Mfawizi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekou Toure, Bahati Msaki amesema lengo la kuleta madaktari hao ili wananchi waweze kuchunguza afya zao na kubaini kama Wanamagonjwa waweze kupata Kinga kabla ya ugonjwa haujaleta madhara mwilini.
" Nawasisitiza watu waje ili wapime na wafahamu afya zao kwani afya ndiyo mtaji wako ukiwa na afya njema utaweza kufanya kazi zako vizuri" amesema Bahati.
Ibrahimu Rimo na Mariamu Mussa ni baadhi ya wananchi ambao wamepewa huduma wameishukru Serikali kwa kuweka kambi hiyo kwani wamepata huduma kwa haraka na gharama nafuu.
"Tunaiomba Serikali iweke utaratibu wa kuleta huduma hizi mara mbili kwa mwaka kwa sababu inasadia kupata huduma kwa wakati na gharama nafuu," Walisema.
0 Comments