Ticker

6/recent/ticker-posts

‘WAKULIMA TUMIENI FURSA YA UWEKEZAJI WA PSSSF'

Na Mwandishi Wetu

Rai imetolewa kwa wafugaji na wakulima wa Mkoa wa Morogoro kutumia fursa mbalimbali zinazotokana na uwekezaji wa PSSSF katika mradi wa machinjio ya kisasa wa Nguru Hills Ranch kilichopo mkoani hapo.

Akitoa rai hiyo wakati wa uzinduzi rasmi wa mradi, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo, Mh. Mashimba Ndaki , alisema mradi huu ni fursa kwa wakulima na wafugaji ambapo watapata soko la uhakika kwa mifugo yao na soko la mazao yanayotumika kutengeneza chakula cha mifugo. “Natumaini wafugaji wetu na wakulima watatumia fursa hii” alisisitiza Mh. Waziri Ndaki.

Akimkaribisha mgeni rasmi katika hafla ya uzinduzi, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Fatma Mwasa, aliishukuru PSSSF kwa kuwa mstari wa mbele katika kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo nchini. “Miradi hii naamini itakuwa imetoa ajira kwa watanzania,” alisema Mh. Mwasa.

Akihutubia katika hafla ya ufunguzi, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa PSSSF, Bw. Aggrey Mulimuka, alisema PSSSF katika kuunga mkono juhudi za Serilkali za kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya viwanda, Mfuko umewekeza katika maeneo mengi ikiwemo Kiwanda cha Kimataifa cha Bidhaa za Ngozi cha Karanga, kilichopo katika Manispaa ya Moshi. “Kiwanda hicho cha bidhaa kitakuwa kikapata ngozi kutoka katika ranch hii tunayotarajia kuizindua leo” alisema Bw. Mulimuka.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA Hosea Kashimba, akifafanua faida za mradi wa Nguru Hills Ranch alisema mradi unatarajiwa kuongeza kipato kwa wafugaji na wakulima kwa kuwapatia soko la uhakika la mifugo yao na mazao ambayo yatatumika kwa kutengeneza chakula cha mifugo. “Mradi huu utaongeza pato la Taifa kwa kupitia kodi mbalimbali kwa Serikali Kuu na Halmashauri” alisisitiza CPA Kashimba.

Kiwanda kikikamilika kitakuwa na uwezo wa kuchinja ng’ombe 100 na mbuzi 1000 kwa siku. Sambamba na hayo kitakuwa kikinunua mifugo kutoka kwa wafugaji na kuinenepesha ili kufikia viwango vya kimataifa. Kiwanda kinatarajiwa kuajiri zaidi ya wafanyakazi 300 na kitazalisha ajira nyingine 1200 ambazo sio za moja kwa moja.


Waziri wa Maendeleo ya Mifugo, Mhe. Mashimba Ndaki (wapili kulia) na viongozi wengine wakipatiwa maelezo kuhusu machinjio ya kisasa ya Nguru Hills Ranch, huko wilayani Mvonero Mkoa wa Morogoro wakati wa uzinduzi rasmi wa mradi huo Desemba 12, 2022.





Waziri wa Maendeleo ya Mifugo, Mh. Mashimba Ndaki (mwenye tai) na viongozi wengine wakinyanyua kitambaa ikiwa ni ishara ya uzinduzi rasmi wa mradi wa Machinjio ya kisasa ya Nguru Hills Ranch huko Mvomero.
Waziri wa Maendeleo ya Mifugo, Mhe. Mashimba Ndaki (aliyesimama) akizungumza wakati wa uzinduzi huo. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwasa na kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini PSSSF, Bw. Aggrey Mulimuka.

Post a Comment

0 Comments