Ticker

6/recent/ticker-posts

WAANDISHI WA HABARI WATEMBELEA HIFADHI YA TAIFA SADAANI, HIFADHI YA KIPEKEE DUNIANI

Kamishna Msaidizi Uhifadhi, Hifadhi ya Taifa ya Saadani, Ephraim Mwamongo (kulia) akiwa katika mstari wa pamoja na wanahabari na watumishi wengine wa hifadhi wakionesha furaha yao kwa kucheza na kuruka baada ya kufika eneo la Mafui.
Ziara ikiendelea.

Kamishna Msaidizi Uhifadhi Ephraim Mwamongo akiwa na Mwandishi Mashaka Kibaya wakiwa kwenye tabaka la ardhi Mufui.

Aliyevaa miwani na kofia kulia ni Kamshna Msaidizi Uhifadhi,Hifadhi ya Taifa ya Saadani, Ephraim Mwamongo akiteta jambo na Mwandishi wa Global TV Ibrahim Kunoga wakati wa ziara ya waandishi wa habari walipotembelea hifadhi ya Taifa ya Saadani. Mwandishi wa Habari Mashaka Kibaya akiwa ndani ya bodi maalumu wakati wa ziara hiyo.

Majadiliano yakifanyika katika ziara hiyo.

Waandishiwa habari wakiwa ndani ya boti wakati wa ziara hiyo.

Muonekano wa eneo la kupumzika katika hifadhi hiyo.



Na Mashaka Kibaya, Tanga.

HIFADHI ya Taifa ya Saadani ni Mbuga pekee ambayo mazingira yake yameungana na Bahari ikiwa na Ikolojia ya mbuga na ile ya bahari huku ikiwa imesheheni wanyama wa aina mbalimbali.

Miongoni mwa Wanyamapori wanaopatikana katika hifadhi hiyo ni Chui, Nyati, Tembo, Pundamilia, Kuro na wengine wengi hivyo si jambo la ajabu kumkuta Simba akiwa anapunga upepo kwenye fukwe za Bahari ya Hindi.

Kivutio kingine kinachoipatia umaarufu mkubwa hifadhi hiyo ni uwepo wa fungu la mchanga 'Mafui'. Aina ya tabaka la ardhi linalopatikana katikati ya maji eneo ambalo ni kina kirefu, sehemu ambayo mazingira yake huvutia wageni kutembelea.

Mambo yanayopatikana ndani ya Mafui, ni viumbe hai kama vile Kasa, mawe aina ya Matumbawe yenye rangi na maumbo tofauti ambayo ni mazalia ya Samaki eneo ambalo kisheria ni sehemu rasmi ya Hifadhi ya Taifa ya Saadani.

Pia kuna mazingira rafiki yenye umbo la bakuli linalowawezesha watalii kuogelea na hata wale wasioweza wanaweza kutumia eneo hilo kujifunza mchezo huo wa kuogelea ambao umetokea kupendwa sana ulimwenguni.

Kwa wageni au watalii hawawezi kulifikia eneo hilo la Mafui ambalo linafahamika kwa jina maarufu la 'Mwali' ambapo waatalazimika kutumia usafiri wa boti ili kwenda kujionea mambo mazuri yenye kupendeza.

Kwa nini Mafui imebeba umaarufu wa jina Mwali? Ni kwa sababu kuna wakati imekuwa ni vigumu sana kuliona tabaka hilo la ardhi lililopo kwenye kina kirefu cha Maji, hadi pale utakapofanikiwa kufuata ratiba maalum ambayo huzingatiwa na watembeza wageni 'Tour Guide.

Kwa vile Mafui inahitaji kufuata ratiba maalum pasipo kuivuruga ndipo kuiona, wale wasiozingatia kanuni zake hushindwa kuliona eneo hilo, hivyo kiasilia ama tamaduni ikafananishwa kana kwamba unataka kumuona bibi Harusi ambapo kuna taratibu maalum ili kuruhusiwa kumuona.

" Kuna wakati kumuona 'Mwali' (Mafui) ni changamoto, utaiona Mafui hadi pale maji yanapokupwa, hivyo wageni wanaotembelea wakifanikiwa kuliona tabaka hilo la ardhi hufurahi sana" anasema Ephraim Mwamongo Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Hifadhi ya Taifa ya Saadani.

Anaongeza kusema Mwali anapoonekana wageni hujawa na furaha ambapo wanaweza kulitumia eneo hilo kwa kuvishana pete za uchumba, harusi na hata kupumzika tu, watu wakipiga picha na kufurahi mandhari mbalimbali yaliyopo.

Katika kumuongezea thamani Mwali (Mafui), Mwamongo alisema, upo mpango wa kujenga Dock Yard ili vyombo vya Usafiri kama boti kuegesha na kuwawezesha wageni kupanda na kusafiri kuweza kwenda kuona Mwali.

Mwamongo anatanabaisha kuwa, Hifadhi ya Taifa ya Saadani imefanikiwa kiwa na vijana mahiri waliobobea katika kuwaongoza na kuhudumia wageni wakiwawezesha kufurahia ziara zao wakihisi hawajapoteza kitu.

Kimsingi Hifadhi ya Taifa ya Saadani inaelezwa kuwa salama na shirikishi kwa wananchi wanaoishi vijiji jirani ambao wamekuwa wakinufaika kwa kupatiwa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Manufaa mengine wanayopata wananchi wa eneo hilo kupitia uwepo wa hifadhi ya Saadani kuimarika kwa hali ya ulinzi na usalama kwenye maeneo yao, ambapo askari waliopo kwenye hifadhi wamekuwa wakihusika kuhakikisha usalama wa jamii.

Vile vile hifadhi hiyo ya Taifa ya Saadani imekuwa fursa adhimu ambapo wenyeji hususani wavuvi wamekuwa wakiitumia kama Soko kuu kwa ajili ya kuuzia Samaki wao kwa kuwa wageni wanaotembelea eneo hilo hushawishika kununua bidhaa hizo kwa wenyeji wao.

Ili kuiwezesha hifadhi yaTaifa ya Saadani kuendesha shughuli zake kwa tija, kazi ya uboreshaji wa miundombinu imeendelea kufanyika na kwa njia ya reli, barabara, ndege na hata maji zimefanyiwa kazi hatua ambayo imelenga kurahisisha usafiri kwa wageni kutoka sehemu tofauti.

Kamishna Msaidizi uhifadhi wa hifadhi ya Taifa ya Saadani, Ephraim Mwamongo anasema, kupitia kituo 'Station' ya reli Mvave wageni wanaweza kufika kwenye eneo la hifadhi hiyo inayoondokea kuwa na umaarufu mkubwa duniani.

Mwamongo anaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwawezesha kupata fedha zilizosaidi kufanya maboresho ya miundombinu.

Ni kupitia fedha za COVID hifadhi hiyo ya Taifa ya Saadani imeweza kunufaika ambapo kwa upande mwingine Mwamongo amemshukuru na kumpongeza Rais Samia kwa hatua yake kufanya Filamu ya Royal Tour.

Kamishna Msaidizi Mwamongo anasema kwamba, Royal Tour ya Mama Samia Suluhu Hassan imekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza idadi ya watalii kwenye hifadhi ya Taifa ya Saadani ambapo anatoa wito kwa watanzania kujenga utamaduni wa kutembelea hifadhi hiyo ya kipekee.

Post a Comment

0 Comments