Waandishi wa habari Mkoa wa Tanga wakifuatilia mafunzo.
********************************
Na Hamida Kamchalla, TANGA.
KUPITIA mradi wa Shule Bora unaotekelezwa na serikali nchini, waandishi wa habari Mkoa wa Tanga wametakiwa kutumia vema kalamu zao na kutimiza wajibu wao kwa weledi na uhakika wakati wa kuhabarisha umma mafanikio ya mradi huo.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Korogwe, Rahel Mhando, ametoa wito huo kwenye mafunzo kuhusu Mradi wa Shule bora kwa Wanahabari na Maofisa habari wa Halmashauri za Mkoa huo, yaliyofanyika wilayani humo.
Mhando aliyekuwa mgeni rasmi wa mafunzo hayo ya siku moja yaliyolenga kuwawezesha wanahabari kutangaza mafanikio ya sekta ya elimu, amesema kwamba mradi huo ni mali ya serikali ya Tanzania lengo likiwa kuboresha elimu ya kuanzia awali, msingi hadi mwanzo wa kidato cha kwanza.
" Tunajengeana uelewa, kutengeneza mahusiano ili kutangaza mafanikio kwa sekta ya elimu, mradi wa Shule Bora ni wa serikali unaolenga kuboresha elimu ya msingi, kila mmoja ana wajibu kutekeleza majukumu yake kwa uhakika na weledi " amesema.
Amesema kwamba, waandishi wa habari wanawajibika kuhabarisha kwa lengo la kujenga, huku akipongeza juhudi za serikali kuona umuhimu wa kuendelea kuboresha sekta ya elimu.
"Kuhabarisha, kuelimisha na hata kukosoa ndio tunachoenda kufanya lengo ni kujenga, tunampongeza Rais kuendelea kuboresha elimu, fedha za 9 disemba zitaenda kujenga mabweni wanafunzi watapata mazingira mazuri na sekta ya elimu kuleta matunda mazuri" amesema.
Afisa elimu Mkoa wa Tanga Newaho Mkisi, amewataka wanahabari kushirikiana na serikali ili elimu kusonga mbele, akiwaeleza kuwa wao ni wadau muhimu wanaopaswa kutumia taaluma yao vyema kutangaza mambo yanayofanyika.
Mikoa tisa iliyofanikiwa kupata ufadhili wa UKaid na washirika wake ambao ni Cambridge education, ADD International na Plan International ni Dodoma, Katavi, Kigoma, Mara, Pwani, Rukwa, Simiyu, Singida na Tanga.
0 Comments