***********************
Na Mwandishi Wetu
Mamlaka Mawasiliano Tanzania imewasihi watumiaji wa huduma za Mawasiliano kutumia msimu huu wa sikukuu za mwisho wa mwaka kuhakiki laini zao za simu, ili kujilinda na uhalifu mtandaoni.
Akizungumza Alhamis wiki hii kwenye kipindi cha runinga, Morning Trumpet kinachorushwa na kituo cha Azam, Meneja wa Kitengo cha Usimamizi wa Huduma za Mawasiliano ya Simu na Intaneti wa Mamlaka hiyo Mhandisi Sadath Kalolo alisisitiza kuwa, zoezi la uhakiki wa laini za simu linalenga kuwasaidia wananchi hasa watumiaji wa huduma za Mawasiliano ya simu na intaneti kuwa salama wakati wote wanapotumia huduma za Mawasiliano.
“Unapohakiki laini zako za simu unajiweka salama wewe na watumiaji wengine wa Mawasiliano, kwa kuwa wale wasiosajili laini wanazotumia kwa utambulisho wao watakosa huduma kwa kuwa ukizifuta namba hizo, zinafungwa,” alisisitiza.
Alielekeza jinsi ya kufanya uhakiki ambapo mtumiaji anapaswa kubofya *106# kisha kufuata maelekezo yanayotolewa kwa menyu yenye maelekezo ya aina tano yaani mosi; kuangalia usajili, pili; kujua namba zilizosajiliwa katika Mtandao mmoja, tatu; namba zilizosajiliwa mitandao yote, nne; kufuta usajili na tano; kuhakiki au kuongeza namba.
Kwa mujibu wa afisa huyo wa TCRA lengo la zoezi hilo ni “kuangalia iwapo usajili la laini umefanyika kwa usahihi, kuhakiki iwapo unatambua laini zote zilizosajiliwa kwa kutumia namba yako ya kitambulisho cha taifa na kurasimishaji namba unazomiliki kwa kuitambulisha namba kuu na namba za ziada,” alisisitiza.
Aliongeza kuwa, mtumiaji wa huduma za Mawasiliano ya simu mara anapobaini uwepo wa namba ngeni kwenye orodha ya menyu ya uhakiki anapaswa kuzifuta mara moja, kwa kuwasiliana na mtoa huduma wa Mtandao anaotumia kupitia namba 100, au kufika kwenye duka la mtoa huduma au wakala wa mtoa huduma wa Mtandao wake.
Akizungumzia muda uliotolewa katika zoezi la uhakiki Kalolo alisisitiza kuwa, zoezi la kuhakiki na kuhamasisha uhakiki lilianza Desemba Mosi mwaka huu na litaendelea hadi Januari 30, 2023 akisisitiza kuwa mara baada ya zoezi la kampeni ya uhamasishaji kukamilika watumiaji ambao namba zao za simu hazitakuwa zimehakikiwa kwa utambulisho wa kitambulisho cha uraia, zitafungwa kwa kuzingatia kuwa sheria inaelekeza kila mtumiaji wa huduma za Mawasiliano ya simu anapaswa kusajili laini yake kwa njia ya bayometria.
Kuhusu watumiaji ambao walisajiliwa laini za simu na watu wengine kwa sababu mbalimbali zikiwemo kutokidhi vigezo vya umri au kukosa namba ya kitambulisho cha uraia, na hivyo kusajiliwa na wazazi, walezi, ndugu, jamaa na rafiki, TCRA ilielekeza wahakikishe wanapata namba ya kitambulisho cha uraia kutoka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na kusajili laini hizo kwa utambulisho wao kwa kuwa kumsajilia mtu mwingine ni kosa isipokuwa mtumiaji mwenye umri chini ya miaka 18.
Mamlaka hiyo aidha, ilisisitiza kuwa, vijana ambao tayari wametimiza umri wa miaka 18 na walisajiliwa laini zao za Mawasiliano ya simu na wazazi au walezi pia wanapaswa kuhuisha usajili kwa kupata namba ya kitambulisho cha uraia, kisha wahuishe usajili kwa kutumia namba ya kitambulisho hicho.
Mtumiaji wa huduma za Mawasiliano mkazi wa jijini Dar es salaam Briton Mosha akizungumzia zoezi la uhakiki alisisitiza kuwa anatambua umuhimu wa zoezi la uhakiki kwa kuwa alibaini namba 3 ambazo hazitambui na kuzifuta kwa kutumia wakala wa mtoa huduma suala ambalo lilimtia wasiwasi kwamba watu asiowatambua walikuwa wakipata huduma za Mawasiliano kwa utambulisho wake.
“Nikajua hawa watakuwa wale jamaa wa ‘ile pesa tuma kwenye namba hii’ maana niliogopa kwamba vipi kama wangefanya uhalifu kwa namba zinazotambuliwa kuwa ni zangu ilhali siyo?,” alibainisha.
Uhakiki wa laini za Mawasiliano ya simu ni mchakato unaohitaji watumiaji wote wa simu za mkononi kusajili kadi zao za Mawasiliano ya simu ya mkononi kupitia menyu ya *106# ambapo mtumiaji anapobaini uwepo wa namba za simu asizozitambua au anazozitambua na hazihitaji anapaswa kuzifuta kwa kupiga simu kwa mtoa huduma wake kupitia namba 100 au kufika kwenye duka la mtoa huduma.
0 Comments