Ticker

6/recent/ticker-posts

TANZANIA KUNUFAIKA NA DOLA BILIONI 1 KUTOKA KOREA


Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akiipongeza Korea kwa kutoa misaada na mikopo yenye mashariti nafuu kwa Tanzania, wakati wa mkutano kati yake na Waziri Ofisi ya Uratibu wa Sera wa Korea, Mhe. Moon-Kyu Bang (hayupo pichani), jijini Dodoma, kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Emmanuel Tutuba.

Waziri Ofisi ya Uratibu wa Sera wa Korea, Mhe. Moon-Kyu Bang, akiiahidi ushirikiano na Serikali ya Tanzania, wakati wa Mkutano na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (hayupo pichani), kulia ni Mwakilishi wa Korea nchini Tanzania wa Benki ya Exim, Bi. Younk young Jo.

Waziri Ofisi ya Uratibu wa Sera wa Korea, Mhe. Moon-Kyu Bang (katikati) akiteta jambo na baadhi ya wajumbe alioambatana nao katika mkutano kati yake na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (hayupo pichani), uliofanyika jijini Dodoma.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WFM)
Na. Peter Haule, WFM, Dodoma

*******************

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Korea kwa kutenga kiasi cha dola za Marekani bilioni 1 zitakazotolewa kwa njia ya mkopo nafuu kwa Tanzania kupitia Mfuko wa Shirika la Maendeleo ya Kiuchumi (EDCF), kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kipindi miaka mitano

Dkt. Nchemba ametoa shukrani hizo jijini Dodoma, alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri anayesimamia uratibu wa masuala ya Sera wa Korea Mheshimiwa Moon-Kyu Bang, alipokutana na kufanya mazungumzo naye akiwa katika ziara ya kikazi nchini.

“Septemba mwaka 2022, Tanzania na Korea tulisaini makubaliano yatakayoiwezesha Tanzania kupata mkopo wenye riba nafuu wenye thamani ya dola za Marekani bilioni moja ambapo Tanzania itakopa mkopo huo kwa riba ya asilimia 0.01 kwa mwaka na kuulipa kwa kipindi miaka 40 ambacho kimeambatana na kipindi cha neema cha miaka 15.” alisema Dkt. Nchemba

Dkt. Nchemba aliishukuru Korea kwa kuahidi pia kusaidia utekelezaji wa miradi miwili mipya ukiwemo mradi wa maji na usafi wa mazingira mkoani Iringa wa Iringa na ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Binguni-Zanzibar, ambayo italeta manufaa makubwa kwa wananchi.

Alisema kuwa Wizara na Serikali kwa Maelekezo na mwongozo wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, ipo tayari kushirikiana na timu ya Serikali ya Korea na wawakilishi wa Benki ya Exim nchini kuweza kukamilisha kwa haraka taratibu zote za kitaalamu ili miradi hiyo iweze kutekelezwa.

Aidha Dkt. Nchemba, amezikaribisha Kampuni za Jamhuri ya Korea kuwekeza nchini ukiwemo uwekezaji wa ubia katika miundombinu wezeshi ikiwemo ya barabara, nishati, afya, usafiri wa majini na Tehama.

Dkt. Nchemba alisema kuwa Serikali ya Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji kwa kuwa ni lango la nchi nchingi zikiwemo za Afrika Mashariki na kusini mwa Afrika na pia ina mazingira bora ya uwekezaji na ufanyaji biashara.

Pia alibainisha kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Korea ni wa kirafiki na kindugu, ikizingatiwa kuwa Serikali ya Korea iliwezesha Tanzania kupata fedha za kutekeleza miradi mingi ukiwemo mradi wa ujenzi wa daraja la Tanzanite jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wake Waziri Ofisi ya Uratibu wa Sera wa Jamhuri ya Korea, Mhe. Moon-Kyu Bang aliahidi kuwa mradi wa kuboresha usambazaji maji na mazingira wa Iringa uamuzi wake wa kuutekeleza utafanyika mwishoni mwa mwaka huu na utekelezaji utaanza mara moja ilihali mradi wa Hospitali ya Rufaa ya Binguni Zanzibar, taratibu za kitaalam zitakamilishwa ndani ya miezi sita ili utekelezwe.

Vilevile ameeleza kuwa Korea inampango wa kuongeza zaidi ya marambili kiwango cha bajeti ya kutoa misaada kwa Afrika hadi kufikia mwaka 2030, hivyo ameitaka Tanzania kuandaa miradi ambayo itatekelezwa katika mpango huo utakapoanza ikiwemo miradi ya ubia na Sekta binafsi katika maeneo ya barabara, reli na mingine.

Mhe. Bang aliipongeza Serikali kwa kutekeleza mradi wa kimkakati wa reli ya kisasa ambao amesema ni kubwa na utasaidia kuinua uchumi wa nchi na nchi Jirani na kuahidi kuwa atazishawishi kampuni kutoka nchini mwake kushiriki katika mradi huo kwa njia ya utaratibu wa ubia kati ya umma na sekta binafsi.

Post a Comment

0 Comments