************************
Na Magrethy Katengu
Shirika la Umeme Tanzania TANESCO limesema limefanikiwa kupunguza makali ya upungufu wa umeme kutoka wastani wa kati ya megawati 200 hadi 250 wiki iliyopita hadi kufikia wastani wa kati ya megawati 100 hadi 150 wiki hii.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mkuu TANESCO Bw.Maharage Chande amesema jitihada zinaendelea kufanyika hivyo tayari wameshakamilisha matengenezo ya mtambo mmoja wa kituo cha Kinyerezi namba II na umeshaanza kuzalisha megawati 45 za umeme ambazo zinaingia kwenye Gridi ya Taifa kuanzia 24 Novemba 2022.
Aidha amesema wamekamilisha pia matengenezo ya mitambo miwili iliyopo katika kituo cha Ubungo namba III na imeshaanza kuzalisha kati ya megawati 35 na 40 za umeme kwenye Gridi ya Taifa kuanzia tarehe 25 Novemba 2022.
"Tumeshakamilisha matengenezo ya mtambo mmoja wa kituo cha Kidatu na umeshaanza kuzalisha megawati 50 za umeme kwenye Gridi ya Taifa kuanzia tarehe 30 Novemba 2022 pamoja na hizo megawati nyingine mtaona kuwa tumeongeza kiasi fulani cha umeme ambacho kitapunguza makali ya mgao wa umeme”Mkurugenzi Chande.
Sambamba na jitihada hizo amesema wamekamilisha ufungaji wa mitambo miwili iliyopo katika kituo cha upanuzi cha Kinyerezi namba I na inaingiza megawati 90 za umeme kwenye Gridi ya Taifa.
Hata hivyo pia amesema bado wanaendelea na jituhada za kuhakikisha kuwa tatizo la uhaba wa umeme linaisha ambapo kwa sasa majaribio ya mtambo mmoja uliopo katika kituo cha Ubungo namba III yanaendelea na utazalisha megawati 20 za umeme kwenye Gridi ya Taifa kabla ya mwisho wa mwezi Disemba 2022
Mkurugenzi Chande amesema pia wanategemea mtambo mmoja uliopo katika kituo cha upanuzi cha Kinyerezi namba I utaanza kuzalisha megawati 45 za umeme kwenye Gridi ya Taifa ifikapo Februari 2023.
"Niseme kuwa pamoja na mvua kuendelea kunyesha kwenye baadhi ya maeneo nchini, lakini bado hali ya kiwango cha maji katika mabwawa ya kuzalisha umeme haijawa ya kuridhisha kwa mfano; kituo cha New Pangani Falls (NPF) kwa sasa kinazalisha megawati 7 badala ya megawati 68, kituo cha Hale kinazalisha megawati 4 badala ya megawati 10.5, kituo cha Kidatu kinazalisha megawati 145 badala ya megawati 204 na bwawa la Nyumba ya Mungu linazalisha megawati 4 badala ya megawati 8. Hali hii inalifanya Shirika kuendelea kutegemea zaidi uzalishaji wa umeme kwa kutumia gesi asilia kuliko kwa kutumia maji” Amesema Chande.
Aidha Shirika litaendelea kutoa taarifa za hali ya umeme pamoja na kutoa ratiba za upungufu wa umeme kupitia tovuti ya http://www.tanesco.co.tz, kwa kuwatumia ujumbe mfupi wa maneno (SMS) na kwenye magroup ya whatsapp ya wateja wake.
0 Comments