Na Sheila Katikula,Mwanza
Serikali imesema itaendelea kusaidia vijana wenye mawazo chanya ya kibiashara ili waweze kutimiza malengo yao na kuweza kulitumikia Taifa ipasavyo.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jenifa Omolo wakati akizungumza na kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba kwenye mahafali ya 36 ya duru ya pili ya chuo Cha Mipango na Maendeleo Vijijini mkoani Mwanza.
Amesema kila kijana anapaswa kujiunga kwenye kikundi vyenye lengo moja ambavyo vimesajiliwa ili waweze kupata fursa mbalimbali na kupelekea kujiajiri wenye na siyo kuwa tegemezi.
"Mkijiunga kwenye vikundi ni rahisi kukabiliana na changamoto ya mtaji tofauti na ukiwa peke yako kwani kidole kimoja hakivunji chawa,"amesema Jenifa.
Amesema kuwa anaamini vijana wanatambua kuwa msingi wa ujasiriamali ni wazo na siyo fedha kwani fedha inakuja baada ya kutekeleza wazo.
Jenifa amesema waliofanikiwa kwenye biashara ni wale waliojaribu mara kadhaa bila kuchoka ni vema
Kila mmoja kuthubutu kufanyia kazi maono na kutoongopeshwa na watu wachache waliokuwa na maono kama yao lakini wakashindwa.
Hata hivyo amewataka wahitimu na wanafunzi wanaoendelea na masomo kuchangamkia fursa ya upendeleo inayotolewa na sheria ya ununuzi wa umma sura 410 kwa makundi maalumu katika jamii hususani vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la uongozi wa chuo hicho Profesa Martha Qorro amesema wamekuwa wakitoa elimu ambayo itawasaidia wahitimu hao watakapokuwa kazini.
"Kwanza wahitimu hawa wanamazoweya ya kukaa na wananchi kutokana na elimu waliyoipata wanaweza kuishi mazingira yoyote na kufanya kazi," amesema Martha.
Mkuu wa chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini, Profesa Hozen Mayaya amesema jumla ya wahitimu 8,916 wamefundishwa na kupata uelewa,maarifa na ujuzi stahiki wakiwemo wanaume 3,922 na wanawake 4,994.
Mayaya amesema Serikali imekuwa ikitoa kipaumbele kwenye elimu hapa nchini kwa kuweka miundo mbinu salama kwa taasisi za elimu ya juu, na shule za Sekondari kwa kufanya ukarabati.
0 Comments