Ticker

6/recent/ticker-posts

KIVUKO CHA MV TANGA UKARABATI TAYARI, CHAANZA KAZI RASMI, KUBEBA ABIRIA 100.


Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe.Omari Mgumba akioneshwa hatua za kivuko na kupata maelezo namna ya kuvitumia.
Muonekano mpya wa Kivuko cha Mv Tanga baada ya kukarabatiwa.
Mkuu wa Mkoa, Mgumba akikata utepe kuzindua kivuko hicho ambacho kitafanya safari zake Bweni- Kipumbwi.


Na Hamida Kamchalla, PANGANI.


SERIKALI kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa kushirikiana na Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) imekamilisha ukarabati wa Kivuko cha Mv Tanga kinachohudumia wananchi wa Wilaya ya Pangani.


TEMESA wamekabidhi kivuko hicho kilichokarabatiwa kwa muda wa miezi sita kutokana na uchakavu wake, kiligharimu zaidi ya kiasi cha sh bilioni 1.1, ambacho kitapanua wigo wa usafirishaji, kimeelezwa kwamba ni muhimu kwa ustawi wa maendeleo ya wakazi wa Pangani lakini kwa Mkoa wa Tanga.


Akipokea kivuko hicho Mkuu wa Mkoa wa Tanga Omari Mgumba amesema kukamilika kwa ukarabati wa kivuko cha Mv Tanga kutasaidia kuboresha huduma za mawasiliano na usafirishaji wa bidhaa za wananchi pamoja na kuchochea maendeleo.


"Kivuko hicho cha Mv Tanga kitainua na kuongeza uboreshaji wa huduma za mawasiliano na usafirishajina kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wetu, nitoe pongezi tena kwa Wizara ya Ujenzi kwa kuwezesha vivuko vipya kujengwa nchini" amesema Mgumba.


Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi sekta ya Ujenzi Ludovick Nduhiye amesema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/23 serikali imepanga kutanua vivuko nane ambavyo vitatoa huduma katika maeneo mbalimbali hapa nchini kiwemo kwenye ziwa Victoria na maeneo yanayohitajika vivuko hivyo kwenye bahari ya hindi.


"Kwa mwaka wa fedha 2022/23 Wizara inatekeleza ujenzi wa vivuko vipya nane, katika vivuko hivyo vipo ambavyo ni pamoja na vitakavyotoa huduma katika ukanda wa ziwa Victoria" amefafanua Nduhiye.


"Kati ya vituo hivi vipya nane, tayari tumeshasaini mikataba ya vivuko vitano, yenye thamani ya sh bilioni 33.2, na malipo ya awali yameshalipwa kwa wakandarasi na sasa hivi kazi za ujenzi zinaendelea" aliongeza.



Awali Mtendaji Mkuu wa TEMESA makao makuu, Lazaro Kihahala amesema kivuko cha Mv Tanga kina uwezo wa kubeba abiria 100 kwa wakati mmoja sambamba na mizigo yenye uzito wa tani 50 yakiwemo magari madogo sita.



Aidha Kihahala amesema kuwa katika mwaka huu wa fedha, serikali imepanga kufanya ukarabati kwa vivuko 14 ambavyo gharama yake itakuwa sh bilioni 22.99.


"Vivuko vitakavyo karabatiwa ni Mv Tanga, ambacho ndiyo hichi tunakabidhi, Mv Misungwi, Mv Musoma, Mv Sabasaba, Mv Kazi, Mv Nyerere, Mv Kitunda, Mv Kilombero II, Mv Ruhuhu, Mv Old Ruvuvu, Mv Magogoni, Mv Ujenzi, Mv Kome II, na Mv Mara" amefafanua.



Waziri wa Maji na Mbunge wa Pangani Juma Aweso baada ya kuishukuru serikali kwa ukarabati wa kivuko hicho, amesema, "tunaiomba serikali isaidie Wilaya hii kupata boti ya mwendo kasi ili kuwezesha kutoa huduma ya uhakika wa safari za Pangani na Zainzar".


Aidha wakazi wa Wilaya hiyo wametoa shukrani zao pamoja na kuipongeza serikali kwa kuwapatia kivuko hicho kwani awali walikuwa wakipata shida ya usafiri kwani waliotumia kivuko kimoja lakini pia ni kidogo.


"Tunaishukuru serikali kutatua kero ya kivuko hicho kwa sasa tutaendelea kujituma na kufanya kazi zetu kwa huru kwa wanauhakika wa kivuko ambazo kitawatoa huduma kwa muda wote" amesema Mariam Mohamedi.


Baada ya kukamilika matengenezo ya kivuko cha Mv Tanga kwa sasa Pangani wana vivuko viwili ambavyo vitatoa hutuma kwanzia asubuhi mpaka saa sita usiku ambapo wananchi hao watakuwa wanavuka eneo la Bweni kuelekea Kipumbwi.

Post a Comment

0 Comments