Ticker

6/recent/ticker-posts

KISHAPU YAJIVUNIA MAFANIKIO MAKUBWA MIAKA 61 YA UHURU

 


Mwonekano wa Jengo la Mionzi katika Hospitali ya Wilaya ya Kishapu
Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya jamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Bwana Joseph Swalala akizungumzia maendeleo mbalimbali yaliyotekelezwa na halmashauri hiyo kuelekea maadhimisho ya Miaka 61 ya Uhuru wa Tanganyika.

Na Stela Paul - Shinyanga.

Kuelekea Maadhimisho ya Miaka 61 ya uhuru wa Tanganyika Disemba 9, 2022 Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga imetaja kupiga hatua mbalimbali za mafanikio katika utoaji wa huduma za kijamii kwa wananchi ikiwemo maboresho ya miundombinu ya sekta ya Afya.


Akizungumza leo Jumatano Disemba 7,2022 wakati Mdahalo wa kuzungumzia maendeleo yaliyotekelezwa na halmashauri ya Kishapu kuelekea Maadhimisho ya Miaka 61 ya Uhuru wa Tanganyika, 
Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya jamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Bw. Joseph Swalala amesema mpaka sasa halmashauri hiyo imefanya maboresho ya miundombinu katika sekta mbalimbali ikiwemo afya ili kuwezesha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi.

Amesema moja ya mafanikio ya kujivunia ni utekelezaji wa sera zinazolenga kuwawezesha wananchi kupata huduma za kijamii kwa urahisi.

“Kutokana na sera nzuri na maendeleo ambayo yamepatikana tangu kupata uhuru miundombinu sasa imeelekezwa iwe rafiki kwa wananchi wote wakiwemo wenye ulemavu, lakini tunaweza kwenda mbali zaidi kwamba kutokana na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi makundi ya watu wenye mahitaji maalumu wameendelea kuwezeshwa kiuchumi”, amesema Swalala.

“Halmashauri ya Kishapu tumeendelea kuzingatia wananchi wote wanapata huduma zote muhimu ikiwemo huduma za afya pamoja na huduma ya maji bila kutembea umbali mrefu, hayo ndio maendeleo ambayo tumeendelea kuyatekeleza”, amesema Swalala.

Kwa upande wake Kaimu Mganga Mfawidhi Dkt. Raymond Tibakya wa Hospitali Wilaya ya Kishapu inayotambulika kwa jina la Dr. Jakaya Kikwete amesema katika kuelekea maadhimisho ya miaka 61 ya uhuru, serikali imeboresha huduma za afya hususani kwa akina mama wajawazito na hivyo kusaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto.

“Hali ya utoaji huduma kwa sasa ikilinganishwa na zamani kuna mabadiliko makubwa sana itukianza na huduma za mama na mtoto zimeboreshwa sana, mwanzo huduma za upasuaji zilikuwa hazipo lakini kwa sasa zinapatikana” ,amesema Dr. Tibakya.

“Kwa sasa hospitali yetu imejengewa majengo mapya ambapo serikali kuu iliweza kutoa fedha kwaajili ya ujenzi wa majengo matano jengo la idara ya dharura, wodi ya watoto, wodi ya kinamama, jengo la maabara pamoja na jengo la mionzi” ,amesema Dr. Tibakya.

Nao baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Kishapu wamepongeza juhudi mbalimbali za maendeleo zinazoendelea kutekelezwa na serikali kuelekea Miaka 61 ya uhuru hali ambayo imesaidia kupunguza changamoto mbalimbali zilizokuwa zinaikumba jamii na kwamba wameiomba serikali kuboresha miundombinu ya barabara katika Wilaya hiyo.

Kuelekea Maadhimisho ya Miaka 61 ya uhuru wa Tanganyika, Halmashauri ya wilaya ya Kishapu kwa kushirikiana na wananchi imeanza kufanya shughuli mbalimbali za kijamii michezo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho hayo Disemba 9, 2022.
Mwonekano wa Jengo la Mionzi katika Hospitali ya Wilaya ya Kishapu
Muonekano wa Hospitali ya Wilaya ya Kishapu
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kishapu Dr. Raymond Tibakya akizungumza maboresho yaliyofanyika katika huduma za kiafya katika hospitali hiyo
Muonekano wa nje wa Hospitali ya Wilaya ya Kishapu
Mkazi wa Wilaya ya Kishapu akizungumza kuelekea maadhimisho ya Miaka 61 ya uhuru wa Tanganyika
Mkazi wa Wilaya ya Kishapu akizungumza kuelekea maadhimisho ya Miaka 61 ya Uhuru wa Tanganyika
Picha ya pamoja baada ya Mdahalo wa kuzungumzia maendeleo yaliyotekelezwa na halmashauri ya Kishapu kuelekea Maadhimisho ya Miaka 61 ya Uhuru wa Tanganyika

Post a Comment

0 Comments