****************
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Camillus Wambura amesema jumla ya watu 23739 wamefanyiwa ukatili wa kijinsia kuanzia kipindi cha Januari hadi Oktoba 2022 ikilinganishwa na watu 25,579 kwa kipindi kama hicho mwaka 2021 ambapo ni upungufu wa watu 1840 sawa na asilimia 3.73.
IGP Wambura amesema hayo Jijini Tanga wakati akifunga Kikao cha Watendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto kutoka mikoa ya Tanzania bara na Zanzibar kilichokuwa kikifanyika jijini humo kwa siku tatu kwa lengo la kufanya tathmini kwa mwaka 2022 na kuweka mikakati kwa mwaka 2023.
Aidha, aliwataka watendaji hao kuhakikisha kuwa kunaendelea kuwepo na usiri katika kushughulikia wahanga wa vitendo vya ukatili nchini na kwa wanaofanya vitendo hivyo waweze kufichuliwa ili lengo la kukomesha vitendo hivyo liweze kutimia sambamba na watendaji hao kujenga taswira chanya ya Jeshi la Polisi kwa jamii jambo ambalo litasaidia kutoa haki kwa Wahanga wote wa matukio hayo.
Naye Mwakilishi wa Shirika la LSF Bi. Jane Matinde amesema kuwa, shirika hilo litaendelea kufadhili mafunzo kwa watendaji hao ili kuwa na watendaji wenye weledi katika dawati ambalo limekuwa mkombozi kwa wanajamii wa Tanzania ambao wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ukatili.
0 Comments