Ticker

6/recent/ticker-posts

FEDHA ZA FIDIA ZITUMIENI KWENYE MAENDELEO ZAIDI.



***********

Na Shemsa Mussa, Kagera .


Katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo Wilaya ya Biharamulo, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Albert Chalamila amewataka wakazi wa Kasozibakaya walioguswa na mradi wa bomba la mafuta kutumia fedha walizolipwa fidia kuzitumia vizuri kwa maendeleo yao.


Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Kasozibakaya amemuagiza Mratibu wa bomba la mafuta kuhakikisha waguswa wote wanalipwa fedha zao na kuwasihi wananchi hao fedha za fidia watakazolipwa kuzitumia vizuri katika shughuli zitakazowaletea maendeleo na kuwaongezea kipato.


“Nawasihi fedha hizi za fidia mtakazopewa zitumieni kujiongezea kipato, fanyeni vitu vya maendeleo, mkizitumia vibaya itakuwa ni hasara,” ameeleza Mhe. Chalamila


Mmoja wa waguswa katika mradi huo Ndg. Saamoja Masubi ameeleza kuwa yeye ni miongoni mwa walengwa ambao hawajasaini mkataba wa malipo lakini anayo maandishi ya awali ya kumtambua kuwa ni mguswa wa mradi. Alielezwa kuwa watafika nyumbani kwao kwa ajili ya kujiridhisha lakini mpaka sasa hawajafika.


Mratibu wa Bomba la mafuta Ndg. Amos Ntambi ameeleza kuwa mguswa wa mradi ni mama yake hivyo anayetakiwa kusaini mkataba ni mama yake ambae ni mgonjwa. Baada ya maelezo hayo Mhe. Chalamila aliagiza kuwa mratibu afike nyumbani kwa mama huyo, ajiridhishe juu ya afya ya mama yake, endapo atadhibitisha kuwa hawezi kusaini ni vema wanafamilia wakatoa maamuzi yatakayoridhia mtoto wa mama huyo kusaini kwakuwa ndiye anayemtunza mama yake.


Pamoja na hayo ameeleza kuwa jumla ya kaya 38 zimegusa na mradi huu na kaya mbili kati ya hizo watajengewa nyumba ambapo hadi sasa walishaonyeshwa eneo watakapojengewa nyumba na wamechagua aina ya nyumba wanazotaka kujengewa. Kuhusu malipo ya fidia kuchelewa amesema kuwa suala hili linasimamiwa na Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na shirika la Petrol Tanzania taratibu zote za kusaini mikataba zilishakamilika wanasubiri kulipwa fedha yao.


Sambamba na hayo alipokea changamoto mbalimbali za wananchi ikiwemo changamoto ya kutokuwa na elimu juu ya mikopo ya akina mama vijana na watu wenye ulemavu ambapo amemuagiza Afisa Maendeleo ya Jamii kufika katika Kata hiyo na kutoa elimu kwa makundi hayo ili waweze kuzitumia fursa hizo kujiletea maendeleo.

Post a Comment

0 Comments