Mkuu wa Mkoa akiuliza maswali kwa msimamizi wa mradi wa ujenzi wa hospitali ya mji ya Korogwe (Magunga).
Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Basila Mwanukuzi akiteta jambo na mkuu wa Mkoa wa Tanga Omari Mgumba kabla hajaanza kukagua jengo la dharura la hospitali ya mji huo (Magunga)
Kaimu Mganga mkuu wa halmashauri ya mji wa Korogwe Dkt. Hery Kilwale kulia akitoa maelezo kwa mkuu wa Mkoa wa Tanga Omari Mgumba.
*********************
Na Hamida Kamchalla, KOROGWE.
MKUU wa Mkoa wa Tanga Omari Mgumba amemuagiza Katibu Tawala mkoani humo Pili Mnyema kuwasimamisha kazi watumishi watano, akiwemo Mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Korogwe Nicodemus Bei baada ya kushtukia upigwaji wa fedha za umma katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Wakati akiendelea kukagua miradi ya maendeleo wilayani humo alisema amechukizwa na kitendo cha Mkurugenzi wa halmashauri ya mji kutosimamia miradi na kukamilika kwa wakati huku baadhi ikitekelezwa kinyume na makubaliano ya serikali.
Mgumba amefafanua kwamba matakwa ya serikali ni kuona kwamba miradi inapofika katika halmashauri inakwisha kwa wakati ili kusuma maendeleo ya Taifa mbele kwani mwisho wa mradi mmoja ndiyo mwanzo wa mradi mwingine.
"Ras, chukueni hawa wote wanaohusika katika suala hili, ukianza na Ded, Ofisa manunuzi, Mhandisi, Ofisa elimu sekondari na huyu Ofisa ardhi, nendeni nao mkafanye uchunguzi pamoja na wote mnaohusika kila mmoja afanye yake,
"Rpc na ninyi mchunguze jinai kwa hawa watu, na wakati huo wasimame kufika kazini wapishe uchunguzi mpaka tutakapo jirdhisha kama hawana hatia basi watarudi katika nafasi zao kuendelea na majukumu yao" amesema Mgumba.
Baada ya kujionea maendeleo ya miradi aliyokagua ambayo ni hospitali ya Wilaya (Magunga), zahanati tatu za Mgombezi, Old Korogwe na Kilole, soko la Kilole pamoja na shule moja ya sekondari ambapo kati ya miradi hiyo mitano haijamalizika.
"Sijaridhishwa na maendeleo haya ya ujenzi wa miradi ya maendeleo, kati ya miradi niliyotembelea ni mradi mmoja tu wa soko ndiyo vizuri, nasema hii haikubaliki na kila ninapokuja kutembelea miradi Ded hayupo, anaumwa, mara amefiwa na kila aina ya sababu" amesema
Mbali na hayo, Mgumba alimuagiza mkuu wa Wilaya ya Korogwe Basila Mwanukuzi kufanya jitihada za kuhakikisha bidhaa zote za mazao zinashushwa katika soko hilo ili kuweza kuwafanya wafanyabiasha kukubaliana na uhalisia.
Agizo hilo limefuatia taarifa iliyowasilishwa na Ofisa biashara wa halmashauri ya mji huo kuwa soko hilo ambalo limegarimu sh bilioni 1.2 limetelekezwa na wafanyabiashara kwa kukataa kufanya biashara zao kwa madai kuwa ni mbali na mji hivyo hakuna wateja.
"Serikali imetupa fedha nyingi kujenga soko hili lakini halina faida, nakuagiza mkuu wa Wilaya, ukisaidiana na kamati yako ya ulinzi, kuanzia sasa ndani ya siku 14 hakuna mfanyabiashara hata mmoja kushusha mazao ya shambani nje ya soko hili, ni lazima magari yaingie kushusha bidhaa zao hapa" amesema.
Naye Ofisa Biashara wa halmashauri hiyo Farjala Msangi amebainisha kwamba kwa upande wao wamefanikiwa kutekeleza mradi wa soko kwa kufikia asilimia 100 ya ujenzi, lakini wafanyabiashara hawataki kulitumia kwa madai kwamba liko mbali hivyo hakuna wateja wanaofika kununua bidhaa.
"Soko hili limekamilika kwa asilimia 100 halina shida kwenye utekelezaji, tumeyapokea maagizo ya kutaka lianze kazi lianze kutumika na kwamba wafanyabiashara washushie mizigo yao hapa, tutalifanya hili kwa nguvu zetu zote kuhakikisha linatekelezeka, soko hili Lina uwezo wa kuchukua wafanyabiashara zaidi ya 100 kwa wakati mmoja" amesema.
0 Comments