Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI NDAKI ATOA TAMKO KUHUSU UTAMBUZI WA MIFUGO KWA KUTUMIA HERENI ZA KIELEKTRONIKI NCHINI


Ndugu wanahabari,

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeridhia ombi la kuongeza muda wa ukomo wa uwekaji wa hereni za utambuzi kwa mifugo kwa hiari kuwa tarehe 31/12/2022 na baada ya hapo hatua za kisheria zitaanza kuchukuliwa dhidi ya waliokaidi.

Ndugu wanahabari,

Tangu mwezi Oktoba, 2021, Wizara ilianza kufanya utambuzi wa mifugo kwa kutumia hereni za kielekroniki na kuisajili kwenye mfumo wa utambuzi ili kurahisisha ufuatiliaji wa mifugo na mazao yake.

Aidha, tarehe 29/09/2022 Wizara ilitangaza tarehe ya ukomo kuwa 31/10/2022 na baada ya hapo Halmashauri zaidi ya 46 zimeweka hereni za utambuzi kwa mifugo zaidi ya 533,683 na kufanya idadi ya mifugo iliyotambuliwa na kusajiliwa kufikia 5,068,617 ambayo sawa na 11% ya lengo la kuweka alama za utambuzi mifugo 45,920,000.

Naomba kuwashukuru sana Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa katika Mikoa na Wilaya ambazo zimeshaanza kutekeleza zoezi la utambuzi wa mifugo. Vilevile, niwapongeze sana wafugaji ambao mifugo yao imetambuliwa na kusajiliwa kwenye mfumo wa utambuzi.

Ndugu wanahabari,

Baada ya kutangaza tarehe ya ukomo wa utambuzi wa mifugo kwa hiari, nimepigiwa simu nyingi kutoka kwa viongozi wa mikoa, wilaya na wafugaji kuomba niongeze muda.

Niwaombe Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kutumia muda huu wa miezi miwili kusimamia uwekaji wa hereni za utambuzi na kusajili mifugo iliyopo kwenye mikoa na wilaya zenu. Pia kwa wafugaji, hakikisheni kuwa ng’ombe, mbuzi, kondoo na punda wako wanawekwa hereni za utambuzi na kusajiliwa kwenye mfumo kabla ya tarehe 31/12/2022.

Ndugu wanahabari na wafugaji wote,

Utambuzi, Usajili na Ufuatiliaji wa Mifugo ni muhimu kwa madhumuni mbalimbali ambayo ni pamoja na:

Njia ya kurasimisha umiliki wa mifugo kwa mfugaji, Kukabiliana na magonjwa ya mlipuko, Kuimarisha koosaafu za mifugo, Kuongeza thamani ya mifugo kwenye masoko, Kuwezesha bima na mikopo kwa wafugaji, Kuwezesha kupatikana kwa urahisi kwa mifugo iliyopotea au kuibiwa, Ni kufanya sensa ya mifugo kwa ajili ya kuiwezesha Serikali na wadau wengine kupanga mipango ya miundombinu, malisho na huduma zingine, Ni takwa la kisheria kulingana na Sheria ya Utambuzi, Usajili na Ufuatiliaji Mifugo ya mwaka 2010 na Kanuni zake za mwaka 2011.

Ndugu wanahabari,

Hereni za utambuzi wa mifugo zina namba (digits) 12 ambazo ni: 255 zinaonesha utaifa wa mfugo, zikifuatiwa na namba za Mkoa, namba za Mamlaka za Serikali za Mitaa, zikifuatiwa na namba zinazoonesha taarifa mfugo na mfugaji.

Namba hizi hutolewa na Serikali na taarifa za eneo, mfugo na mfugaji hutunzwa kwenye barcode ambazo hupatikana kielektroniki duniani kote. Hereni hizi za kieletroniki ni mali ya Serikali, haziruhusiwi kuuzwa madukani.

Aidha, hereni hutengenezwa na kusambazwa kulingana na mahitaji ya Halmashauri husika. Bei elekezi ya hereni ni shilingi 1,750= ambayo ni gharama kwa ng’ombe na punda na shilingi 1000= kwa mbuzi na kondoo na gharama hizi hulipwa na mfugaji mwenyewe.

Ndugu wanahabari,

Wizara imekuwa ikifanya mafunzo na uhamasishaji kwa wataalam wa mifugo na wafugaji juu ya utambuzi wa mifugo na kazi hii ni endelevu. Uwekaji wa hereni unaendelea nchi nzima katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na mashamba ya mifugo (ranches).

Hadi kufikia leo tarehe 31/10/2022, mifugo iliyowekwa hereni za utambuzi na kusajiliwa ni 5,068,617 kwa mchanganuo ufuatao:

Ng'ombe 4,239,985 sawa na asilimia 18.4 ya lengo, Punda 66,433 sawa na sawa na asilimia 16 ya lengo, Mbuzi 511,930 sawa na asilimia 3 ya lengo, Kondoo 250,269 sawa na asilimia 4 ya lengo. Aidha, Mkoa wa Mbeya unaoongoza kwa kuweka alama za utambuzi mifugo 1,132,468, ukifuatiwa na mikoa ya Tabora 525,093, Rukwa 494,895, Kagera 287,097 na Katavi 286,568. Mikoa ambayo haijafanya vizuri kwenye utambuzi ni Singida mifugo 1,646, Tanga 3,910, Ruvuma 4,672, Njombe 5,300 na Mara 16,012.

Naomba kuwakumbusha tena viongozi wa mikoa, wilaya na wafugaji kuweka alama za utambuzi kwa mifugo na kuisajili kwenye mfumo wa utambuzi.

Ndugu wanahabari,

Kulingana na Mwongozo wa utambuzi, usajili na Ufuatiliaji wa mifugo, wa mwaka 2021, Mamlaka za Serikali za Mitaa zinaweza kufanya utambuzi kwa kutumia wataalam wao wa mifugo au zinaweza kutumia Kampuni binafsi za kutoa huduma za mifugo ambazo ziko takribani 30 nchini.

Wizara imebaini changamoto kwa baadhi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa kufanya uvishaji wa hereni kuwa chanzo cha mapato kiasi cha kuzifanya kampuni nyingi binafsi za kuvalisha hereni kushindwa kuendesha zoezi kama zinavyokuwa zimeingia mikataba na Halmashauri husika.

Niwakumbushe Wakurugenzi Watendaji kuwa hii ni huduma kwa wafugaji kama huduma nyingine kwa wananchi na mfugaji anachangia shs 1750= kwa ng’ombe na punda, na shs 1000= kwa mbuzi na kondoo.

Ndugu wanahabari,

Mwisho, suala la utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo ni muhimu kwa ustawi na maendeleo ya Sekta ya Mifugo nchini. Pia ni sharti la kisheria, hivyo kila Mamlaka za Serikali za Mitaa na wafugaji kuhakikisha mifugo yote kwenye Wilaya inawekwa hereni za utambuzi na kusajiliwa kwenye mfumo wa utambuzi wa taifa.

Aidha, hereni za kielektroniki za utambuzi ambazo zimeshatengenezwa na kuchapishwa zinatosheleza mifugo yote 45,920,000 inayotegemea kutambuliwa.

Hivyo, niziombe Idara za Mifugo kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha mnachukua hereni za utambuzi na kuwafikishia wafugaji kabla ya tarehe 31/12/2022 ili kuepuka usumbufu usiokuwa wa lazima.

Vilevile, elimu na uhamasishaji wa utambuzi wa mifugo kwa wafugaji ni suala endelevu, hivyo kila mtaalam wa mifugo awajibike kuendelea kuwaelimisha wafugaji kuhusu utambuzi na usajili wa mifugo.

Asanteni kwa kunisikiliza

Imetolewa na Mhe. Mashimba Mashauri Ndaki (MB) WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI

Post a Comment

0 Comments