Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MKUU MAJALIWA MGENI RASMI KONGAMANO LA UHAMASISHAJI NA KUKUZA UWEKEZAJI NCHINI

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Bw.John Mnali akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) leo Novemba 28,2022 Jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo UNDP, Bw.Emmanuel Nnko akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) leo Novemba 28,2022 Jijini Dar es Salaam,

*******************

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Kongamano maalum la kuhamasisha na kukuza Uwekezaji na biashara kwa sekta kipaumbele zenye mlengo wa maendeleo endelevu Tanzania, litakalofanyika Novemba 30,2022 Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Waandishi wa habari leo Novemba 28,2022 Jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Bw.John Mnali amesema lengo la mkutano huu ni kutangaza fursa za biashara na uwekezaji zenye mlengo wa maendeleo endelevu zilizopo hapa nchini kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa kutoka nchi mbalimbali duniani.

Amesema Kongamano hilo linatarajiwa kuhudhuriwa na wawekezaji wa Makampuni 100 yatakayohudhuriwa moja kwa moja na kwa njia ya mtandao kutoka nchi mbalimbali duniani.

"Fursa ambazo zipo katika sekta za kipaumbele zenye mlengo wa maendeleo endelevu ni pamoja na sekta ya Kilimo na chakula, Miundombinu, Nishati, Elimu, huduma na na nyingine nyingi". Amesema

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo UNDP, Bw.Emmanuel Nnko amesema kutokana na wawekezaji wengi kushiriki katika kongamano hilo, itasaidia kuiweka na kuitangaza Tanzania kama miongoni mwa maeneo yenye fursa na mazingira mazuri ya kibiashara kwa kampuni mbalimbali duniani.

Aidha amesema kutakuwa na sesheni ya B2B ambapo makampuni ya Tanzania yatapata fursa ya kuongea na Makampuni makubwa yatakayohudhuria na kupata nafasi ya kufanya biashara pamoja na kuweza kuingia ubia katika uwekezaji.

Hata hivyo amesema pia katika Jukwaa la uwekezaji kutakuwa na fursa za kutoa wasilisho la fursa za uwekezaji zinazoendana na malengo endelevu.

"Kongamano hilo halina kiingilio lakini tungependa wale wote ambao wangependa kuhudhuria kutuma uthibitisho. Tunaomba wote waliothibitisha kuhudhuria kufika bila kukosa fursa hii muhimu kwa nchi na wawekezaji wetu". Amesema.

Kongamano hilo limeandaliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Taifa linaloshughulikia maendeleo la UNDP na Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara.

Post a Comment

0 Comments