Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), CPA. Hosea Kashimba, amepata tuzo ya kuwa Mtendaji Mkuu Bora wa mwaka 2022 kwa upande wa Taasisi za Umma nchini.
Utoaji wa tuzo hizo uliratibiwa na taasisi ya kimataifa ya KPMG yenye uzoefi wa miaka 35 katika masuala ya Bima, Fedha, Sheria na Kodi. Tuzo hizo zilitolewa katika ukumbi wa mikutano wa Mlimani City Novemba, 2022 jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo watendaji wa taasisi mbalimbali.
Akizumgumza baada ya kupokea tuzo hiyo, CPA. Kashimba alisema, “Naelekeza tuzo hii kwa wanachama wa PSSSF, hii ni zawadi yao ya kufungia mwaka, hakika tuzo hii inanipa nguvu ya kuwatumia vyema zaidi wanachama mwaka 2023”.
CPA. Kashimba ni mhitimu wa Chuo Kikuu Mzumbe ambako alitunukiwa Shahada ya Uzamili katika Uongozi wa Biashara (MBA Corporate), pia amesomea uhasibu katika Chuo cha Maendeleo ya Uongozi (IDM Mzumbe) na kuhitimu Stashahada ya Juu ya Uhasibu. Pia CPA. Kashimba amehudhuria mafunzo mbalimbali ndani na nje ya nchi.
CPA. Kashimba ni mwanachama wa Institute of Directors Tanzania (IoDT) na mjumbe wa Bodi kwenye taasisi mbalimbali ikiwa pamoja na Benki ya CRBD. Kabla ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Bw. Kashimba ameshakuwa Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Ndani katika uliokuwa Mfuko wa Pensheni wa PPF. Bw. Kashimba aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kuwa Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF kuazia tarehe 19 Februari, 2019.
KPMG hutumia vigezo vingi ikiwemo uongozi bora na unaoacha alama katika sehemu unayoongoza na kwa jamii kwa jumla ili kuweza kumpata mtendaji bora.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) CPA. Hosea Kashimba (kulia) akipokea tuzo ya kuwa CEO bora kutoka kundi la taasisi za umma kwa mwaka 2022, kwenye hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam Jumapili usiku wa kuamkia leo Jumatatu Novemba 28, 2022. Tuzo hizo zimeanzdaliwa na KPMG.
CPA. Hosea Kashimba akionyesha tuzo hiyo.
CPA. Hosea Kashimba akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watendaji wa Mfuko huo.
Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA Hosea Kashimba, akitoa shukrani zake baada ya kupokea tuzo hiyo.
CPA. Hosea Kashimba akiwa ameketi na tuzo yake.
Baadhi ya watendaji wa PSSSF waliohudhuria hafla hiyo.
0 Comments