Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Zanzibar Mhe. Dkt Khalid S. Mohamed (wa tatu kulia) muda mfupi kabla ya kutekeleza ufunguzi wa Mkutano wa Kamati ya Uchumi ya Umoja wa Mamlaka za Udhibiti wa Mawasiliano Kusini mwa Afrika (CRASA), ulioanza Jumatatu Novemba 21, 2022, Unguja. Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Dkt Jabiri Bakari ambao ni wenyeji wa Mkutano huo, wa pili kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara na wa kwanza kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TCRA Mhandisi Othman Khatib. PICHA NA TCRAWaziri wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Zanzibar Mhe. Dkt Khalid S. Mohamed (wa pili kushoto) akiondoka ukumbini muda mfupi baada ya kutekeleza zoezi la ufunguzi wa Mkutano wa Kamati ya Uchumi ya Umoja wa Mamlaka za Udhibiti wa Mawasiliano Kusini mwa Afrika (CRASA), ulioratibiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kufanyika unguja. Picha na TCRA.
Maafisa wa Mamlaka za Udhibiti wa Mawasiliano za Tanzania na Zimbabwe wakifuatilia mada wakati wa Siku ya Kwanza na Mkutano na Semina kwa Kamati ya Uchumi (ERC) ya Chama cha Wadhibiti wa Mawasiliano Kusini mwa Afrika (CRASA), unaofanyika Unguja, Zanzibar chini ya uratibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA). Mkutano huo ulifunguliwa na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Mhe. Dkt Khalid S. Mohamed. Picha na TCRA.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TCRA Mhandisi Othman Sharif Khatib akifuatilia mwenendo wa matukio wakati wa ufunguzi wa Mkutano na Semina kwa Kamati ya Uchumi (ERC) ya Chama cha Wadhibiti wa Mawasiliano Kusini mwa Afrika (CRASA), unaofanyika Unguja, Zanzibar. Mkutano huo ulifunguliwa na Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Zanzibar Mhe. Dkt Khalid S. Mohamed. Picha na TCRA
Wawakilishi wa Mamlaka za Udhibiti wa Mawasiliano za Madagascar na Malawi wakifuatilia mwenendo wa matukio wakati wa ufunguzi wa Mkutano na Semina kwa Kamati ya Uchumi (ERC) ya Chama cha Wadhibiti wa Mawasiliano Kusini mwa Afrika (CRASA), unaofanyika Unguja, Zanzibar. Kutoka kushoto ni Meneja wa Idara ya Masuala ya Uchumi ya Mamlaka ya Mawasiliano Malawi Bi. Linda Kambale, na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Madagascar Bw. Brillant Rakotoratsimanjefy. Picha na TCRA
Maafisa Waandamizi kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Msumbiji (INCM) Bw. Lucio Cardoso (wa kwanza kushoto), Bw. Abdul Amid (katikati) na Oliveira Joaquim Zindoga (wa kwanza kulia), wakifuatilia mada wakati wa semina ya Mafunzo kuhusu bei za Mawasiliano na uchambuzi wa Taarifa za sekta ya Mawasiliano iliyowasilishwa na wawezeshaji (hawamo pichani) kutoka Shirika la Mawasiliano Duniani (ITU). Semina hiyo ya siku nne imeandaliwa na Chama cha Wadhibiti wa Mawasiliano Kusini mwa Afrika (CRASA) kwa ushirikiano na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), na kufunguliwa Jumatano Novemba 21, 2022 na Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Zanzibar Mhe. Dkt Khalid S. Mohamed. Picha na TCRA
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Dkt Jabiri Bakari akiwasilisha hotuba ya ukaribisho kwa wajumbe wa Mkutano wa Kamati ya Uchumi ya Umoja wa Mamlaka za Udhibiti wa Mawasiliano Kusini mwa Afrika (CRASA), ulioanza Jumatatu Novemba 21, 2022, ukifanyika Unguja, Zanzibar; Mkutano huo ulifunguliwa na Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Zanzibar Mhe. Dkt Khalid S. Mohamed. Picha na TCRA
Ofisa wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Bw. Nelson Mwalongo (kulia) akimsajili Ofisa wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi-Zanzibar Mhandisi Issa Hamad Bakar, wakati wa siku ya kwanza ya Semina ya mafunzo ya uchambuzi wa taarifa za mawasiliano iliyoandaliwa na Kamati ya Uchumi ya Umoja wa Mamlaka za Udhibiti wa Mawasiliano Kusini mwa Afrika (CRASA) na kufanyika Unguja, Zanzibar. Semina hiyo ilifunguliwa na Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi-Zanzibar Mhe. Dkt Khalid S. Mohamed. Picha na TCRA
Afisa Habari wa Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Bw. Kassim Salum Abdi.
********************
Yaahidi kufanyia kazi mapendekezo ya Mamlaka za Usimamizi wa Mawasiliano Kusini mwa Afrika;
Waziri apongeza utendaji kazi wa CRASA.
*******************
Na Mwandishi Wetu
Tanzania itashirikiana na nchi nyingine za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), ili kuboresha huduma za Mawasiliano ikiwemo kupunguza gharama za mawasiliano kwa watumiaji wanaovuka mipaka (roaming costs) kwenye wanachama wa chama cha Mamlaka za Udhibiti wa Mawasiliano Kusini mwa Afrika (CRASA).
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa pili wa Kamati ya Uchumi (ERC) ya Chama cha Wadhibiti wa Mawasiliano Kusini mwa Afrika (CRASA) ulioratibiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kufanyika Unguja visiwani Zanzibar, Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi-Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mheshimiwa Dkt. Khalid Mohamed alisisitiza kuwa Serikali itatathmini pendekezo la CRASA juu ya kupunguza gharama za Mawasiliano kwenye ukanda wa nchi za Kusini mwa Afrika.
“Kuhusu suala la roaming kama ulivyolizungumzia (akimlenga Mwakilishi wa Katibu Mtendaji wa CRASA Bw. Shukya Kiroga), sisi pamoja na wenzetu tutaangalia namna ambavyo tutaweza kulitekeleza suala hilo ili kuwezesha wananchi wetu kupata gharama nafuu za Mawasiliano wanapokuwa kwenye nchi wanachama wa SADC,” alisisitiza Waziri Mohamed.
Mkutano huo unaofanyika kwa siku Tano utatanguliwa na Semina inayolenga mbali na mambo mengine kuwajengea washiriki uwezo katika ukusanyaji, uchambuzi na utoaji taarifa za viashiria vya ukuaji wa sekta ya Mawasiliano, chini ya uwezeshaji wa Shirika la Mawasiliano Duniani (ITU).
Akizungumzia ajenda za vikao hivyo Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dkt. Jabiri Bakari alibainisha kuwa wajumbe wa CRASA watapata fursa ya kuelewa masuala muhimu katika ukuzaji sekta ya Mawasiliano, na kwamba TCRA kama mwanachama hai wa CRASA itapata uelewa wa masuala muhimu yatakayosaidia usimamizi Madhubuti wa sekta ya Mawasiliano.
“Huu ni Mkutano muhimu sana na tunatarajia washiriki wote tukiwemo TCRA kurejea nyumbani tukiwa tumeshibishwa elimu katika maeneo bayana. Ikumbukwe kwamba kwenye Mkutano huu, washiriki watajengewa uwezo kuhusu upangiliaji gharama za vifurushi vya mawasiliano ili kuongeza uelewa wa nchi wanachama hatimae kukuza ufanisi wa utoaji huduma za Mawasiliano katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na sisi hapa kwetu tutanufaika sana,” aliweka bayana Mkurugenzi Mkuu wa TCRA.
Nae Kaimu Katibu Mtendaji Mkuu wa CRASA Bw. Shukya Kiroga, ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Kielektroniki wa CRASA, akizungumzia hatua zilizofikiwa katika kuhakikisha nchi wanachama wa CRASA zinafikia muafaka kuhusu kulinganisha masharti ya gharama za huduma za Mawasiliano alisema kuwa, utafiti wa kitaalamu wa gharama elekezi tayari umekamilika na kinachotakiwa sasa ni nchi wanachama kuanza utekelezaji. Aidha, alitoa angalizo kwamba Utekelezaji unahitaji makubaliano ya nchi wanachama ili kufanyika bila mkwamo wakati Utekelezaji wake utakapoanza.
“Ni muhimu sana nchi wanachama wote wakakubaliana, sisi kwa upande wetu tumetekeleza wajibu wetu kinachosubiriwa ni nchi wanachama waridhie kisha utekelezaji wake uanze; hii nikiamini itapunguza pakubwa gharama za Mawasiliano kwenye eneo la Kusini mwa Afrika hasa nchi wanachama,” aliongeza.
Chama cha Wadhibiti wa Mawasiliano Kusini mwa Afrika (CRASA) kinazileta pamoja Mamlaka Kumi na Tatu za Usimamizi wa Mawasiliano Kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo ni Tanzania (Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Zambia (Mamlaka ya Habari na Teknolojia ya Mawasiliano (ZICTA)), Zimbabwe(Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Posta (POTRAZ)), Afrika Kusini (Mamlaka Huru ya Mawasiliano (ICASA)),
Msumbiji (Taasisi ya Taifa ya Mawasiliano (INCM)), Namibia (Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Namibia (CRAN)), Eswatini (Kamisheni ya Mawasiliano (ESCCOM)), Malawi (Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Malawi (MACRA)), Angola (Mamlaka ya Mawasiliano Angola (INACOM)), Botswana, Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Botswana (BOCRA) na Congo, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Posta na Simu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, nyingine ni Mamlaka ya Mawasiliano na Teknolojia Mauritius na Mamlaka ya Mawasiliano Lesotho (LCA).
0 Comments