*Huduma zote za Mfuko ni bure
Na Mwandishi Wetu, Mwanza
Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umetoa wito kwa Wastaafu na Wanachama wote kuwa makini na wimbi la matapeli wanaotoa taarifa za uongo kwa Wananchama wake kwa lengo la kujipatia kipato kwa njia zisizo halali.
Kauli hiyo imetolewa na Afisa Uhusiano Mkuu wa PSSSF, Bw. Abdul Njaidi,katika Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha yanayoendelea katika viwanja vya Rocky City Mall jijini Mwanza na kuhudhuriwa na watu mbalimbali kwa lengo kupata elimu.
Afisa Uhusiano Mkuu wa PSSSF, Bw. Abdul Njaidi akitoa elimu katika semina iliyoandaliwa na Wizara ya Fedha katika maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha yanayoendelea jijini Mwanza.
Afisa Uhusiano Mkuu wa PSSSF, Bw. Abdul Njaidi akitoa elimu katika semina iliyoandaliwa na Wizara ya Fedha katika maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha yanayoendelea jijini Mwanza.
*******
Katika maonesho hayo, Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na washiriki mbalimbali huendesha darasa kila siku kwa lengo la kutoa elimu kwa kina juu ya sekta inayotoa elimu kwa siku husika, ambapo Bw. Njaidi alitumia siku ya darasa la Hifadhi ya Jamii kutoa tahadhari juu ya uwepo wa matapeli wanaowalenga Wastaafu na Wanachama wa PSSSF. Kauli mbiu ya Maadhimisho hayo ni, Elimu ya Fedha kwa Maendeleo ya Watu.
“Kumekuwa na wimbi kubwa la matapeli ambao wanawalenga Wastaafu wetu, kwa kuwarubuni kwa lengo la kujipatia fedha kutoka kwa Wastaafu wetu hao, jambo ambalo sio zuri hata kidogo” alifafanua Bw. Njaidi.
Mkurugenzi wa Fedha wa PSSSF, Bi. Beatrice Lupi., akitoa huduma kwa mmoja wa wanachama waliofika katika banda la PSSSF
***********
Bw. Njaidi alisema huduma za PSSSF ni bure na hakuna huduma inayolipiwa na kuwataka wanachama wanapopigiwa simu za kuwataka kutoa fedha watoe taarifa Polisi au katika ofisi za PSSSF ambazo zipo kila Mkoa Tanzania, ikiwemo na ofisi ya Zanzibar.
“Kanda ya ziwa mnapaswa kuwa makini zaidi, kwani kuna mtuhumiwa mmoja anayedaiwa kujihusisha na kutapeli Wastaafu ambaye alitiwa mbaroni jijini hapa” alifafanua Bw. Njaidi.
Katika Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha, watu wanaotembelea katika banda la PSSSF ambalo lipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu wanajipatia huduma mbalimbali ikiwemo; elimu juu ya Hifadhi ya Jamii, mafao yatolewayo na PSSSF, kujihakiki, kuangalia taarifa za michango yao, kufuatilia mafao yao na kupata taarifa mbalimbali za uwekezaji wa Mfuko.
Kamishina wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya fedha katika wizara ya fedha na Mipango, Dkt. Charles Mwamwaja akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kutembelea banda la PSSSF katika Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha.
************
“Kwa kweli wanachama wa Mfuko wanajitokeza kupata huduma mbalimbali, mpaka sasa wengi wanaofika wanahitaji kujua juu ya taarifa zao za michango. Pia katika banda letu tunatoa elimu ya huduma ya PSSSF kiganjani ambayo ni njia rahisi kwa wanachama kufuatilia huduma mbalimbali za Mfuko kupitia simu yake ya kiganjani” alieleza Bw.Njaidi.
PSSSF imekuwa ikishiriki katika maonesho mbalimbali kwa lengo la kutoa elimu kwa umma juu ya huduma na bidhaa zinazotolewa kwa Wanachama na Watanzania kwa jumla.
0 Comments