******************
Benki Kuu ya Tanzania imebaini kuwa kuna baadhi ya taasisi, kampuni na watu binafsi wanaojihusisha na biashara ya kutoa mikopo bila ya kuwa na leseni, jambo ambalo ni kinyume na Kifungu cha 16(1) cha Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018.
Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuutaarifu Umma kuwa taasisi, kampuni na mtu binafsi wasio na leseni husika hawaruhusiwi kufanya biashara ya kukopesha.
Aidha, kwa mujibu wa Kifungu cha 16(2)(a) cha Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018, hatua zitakazochukuliwa kwa ukiukaji wa Sheria hiyo ni pamoja na faini isiyopungua Shilingi Milioni 20 au kifungo kwa muda usiopungua miaka miwili.
Sambamba na tangazo hili, Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuwaasa wananchi kuepuka kukopa au kufanya biashara na taasisi, kampuni au mtu binafsi ambao hawana leseni.
Aidha, orodha ya taasisi, kampuni na watu binafsi wenye leseni za biashara ya kukopesha zilizotolewa na Benki Kuu ya Tanzania inapatikana kwenye tovuti ya Benki Kuu ambayo ni www.bot.go.tz.
0 Comments