Ticker

6/recent/ticker-posts

KAIRUKI : WASILISHENI NYARAKA ZA KIUTAWALA ZINAZODAIWA KUUNGUA


Angela Msimbira DAR ES SALAAM 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Angellah Kairuki ameubana uongozi wa soko kuu la Kariakoo kwa kuwataka kuwasilisha nyaraka zote muhimu za kiutawala zinazodaiwa ziliungua na moto kwenye tukio lililotokea Julai 10, mwaka jana. 

Akizindua Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Masoko ya Kariakoo leo Novemba 15, 2022 Jijini Dar Es Salaam, Waziri kairuki amewataka waliofanya udanganyifu wa aina yoyote, kujisalimisha mara moja kwa kusa serikali ina mkono mrefu wa kuzipata nyaraka hizo wakati wote. 

Amewataka watendaji hao kujisahihisha kama kuna taarifa walizoficha kwa kuziwasilisha kwake mapema iwezekanavyo kwa sababu hakuna atakayesalia katika hilo. 

Alisema jambo hilo wameliachia vyombo vya uchunguzi kufanya kazi yake na ndio sababu anahimiza watendaji hao kujisalimisha mapema. 

"Bado mna nafasi, mkifikiri majibu mliyotoa wakati ule kuwa ndio tumemalizana, bado hatujamalizana ni bora tujisalimishe haraka kuliko kukaa kimya, hela ya serikali haiwezi kupotea hivi hivi tu, pia kama kulikuwa na hujuma itajulikana, kama ni moto wa 'Nature Desaster' itajulikana," amesema Kairuki. 

Waziri Kairuki ameitaka bodi hiyo ya wakurugenzi kufanyia kazi hoja zote za ukaguzi na kufanyia kazi yale yote yaliyobainika. 

Sambamba na hilo, amesisitiza kufanya mapitio ya umiliki wa asilimia 51 ya hisa za soko hilo zinazomilikuwa na Jiji la Dar es Salaam ambayo awali ilijumuisha halmashauri zote za Mkoa huo lakini sasa zinamilikiwa na Ilala pekee. 

Amewataka muundo wa kiutendaji wa shirika hilo ukaguliwe ili kuongeza ufanisi wa kiutendaji wa soko hilo. 

Waziri Kairuki ameagiza kuangalia mifumo ya TEHAMA kama inasaidiaje kutunza na kuhifadhi nyaraka, usimamizi wa makusanyo na matumizi ya fedha. 

Amewataka kufanya ukaguzi wa ujenzi kama thamani ya fedha na kazi inayofanyika, asilimia 49 ulipofikia ujenzi na maendeleo yake. 

Awali, Kaimu Meneja Mkuu wa Masoko ya Kariakoo, Sigsibert Valentine, akiwasilisha taarifa kwa Waziri Kairuki, amesema ujenzi wa soko hilo unaojumuisha ukarabati wa jengo la zamani na ujenzi wa jengo hilo mpya, umefika asilimia 49. 

Amesema ujenzi huo utakamilika Oktoba 23, 2023 ambalo litakuwa naj uwezo wa kuajiri watu 4,000 tofauti na awali liliajiri 1,600.

Post a Comment

0 Comments