Ticker

6/recent/ticker-posts

AFRIKA KUSINI YAISHUKURU TANZANIA KUHIFADHI MAENEO YA HISTORIA YA NCHI HIYO


**********************

Na Shamimu Nyaki

Serikali ya Afrika Kusini imetoa pongezi na shukrani kwa Tanzania kwa kuendelea kuhifadhi na kulinda maeneo ya Historia ya wapigania Uhuru wa nchi hiyo yaliyoko Mazimbu mkoani Morogoro.

Pongezi na Shukrani hizo zimetolewa na Naibu Waziri wa Michezo, Sanaa na Utamaduni wa Afrika Kusini, Mhe. Nocawe Mafu wakati alipozungumza katika mdahalo wa mashuhuda wa wapigania Uhuru wa nchi hiyo, ikiwa ni siku ya pili ya Tamasha la Afrika Kusini linaloendelea nchini Novemba 19, 2022.

"Afrika Kusini na Tanzania ni ndugu, tumeshuhudia jinsi mnavyoenzi undugu huu, tumefurahi kuona mnavyotunza na kulinda maeneo ya Urithi wa Ukombozi wa Bara letu zaidi nchi yetu, nawaahidi makubaliano ya ushirikiano wetu yote tutayatekeleza", amesema Mhe. Nocawe.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Alberto Msando akiwasilisha salamu kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, amesema kuwa nchi hizo zinashirikiana katika Sekta nyingi ambapo waasisi wa nchi hizo Baba wa Taifa Hayati Julius Nyerere na Nelson Mandela walihakikisha nchi hizo zinakuwa huru na pamoja na Bara zima la Afrika.

Mhe. Msando alitumia nafasi hiyo kuwaongoza Naibu Waziri huyo, Balozi wa Afrika Kusini hapa nchini, Mhe. Nolurthando Malepe na Raia wa Taifa hilo kutembelea Kambi ya wapigania Uhuru wa nchi hiyo pamoja na makaburi waliozikwa Mashujaa waliopigania Uhuru wa Taifa hilo.

Ziara hiyo ni katika siku ya pili ya Tamasha la Utamaduni wa Afrika Kusini na Tanzania wenye lengo la kuimarisha uhusiano katika Sekta ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mkataba wa Ushirikiano katika Sekta ya Utamaduni uliosainiwa mwaka 2011.

Post a Comment

0 Comments