Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax amekutana na kufanya kikao na watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Zambia tarehe 13 Oktoba 2022 katika ofisi za ubalozi huo Jijini Lusaka, Zambia.
Mhe. Tax amekutana na watumishi wa Ubalozi huo baada ya kuwasili nchini Zambia kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa 10 wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia ngazi ya Mawaziri utakaofanyika tarehe 14 Oktoba 2022.
Akiongea katika kikao na watumishi hao Mhe. Waziri Tax ameeleza kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia ni wa kihistoria na kidugu uliojengwa kupitia ujirani mwema na misingi imara iliyowekwa na waasisi wa Mataifa hayo mawili Hayati Baba wa Taifa la Tanzania Mw. Julius Kambarage Nyerere na Hayati Keneth Kaunda wa Zambia. Kupitia kikao hicho, Mheshimiwa Waziri Tax ameelekeza Ubalozi kuendelea kuwa kiungo katika kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa kufuata misingi iliyowekwa na Waasisi wa Mataifa hayo.
“Fanyeni kazi kwa bidii hususan wakati huu tunapotekeleza diplomasia ya uchumi ili ushirikiano wetu uweze kuleta ukombozi wa kiuchumi kwa maslahi mapana ya nchi yetu”alisema Mhe. Waziri Tax.
Naye Balozi wa Tanzania nchi Zambia anayemaliza muda wake Mhe. Hassan Yahya Simba akisoma taarifa ya utekelezaji, ameeleza kuwa ubalozi unaendelea kusimamia ushirikiano wa mataifa hayo mawili kwa kuhakikisha unafatilia kwa karibu maslahi ya Taifa na maslahi ya Watanzania wanaoishi na kuingia nchini Zambia kwa shughuli mbalimbali.
Pamoja na mambo mengine Mhe. Dkt. Tax ametumia nafasi hiyo kutembelea majengo yanayomilikiwa na ubalozi wa Zambia pamoja na ofisi za Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) zilizopo jijini Lusaka, Zambia.
Ubalozi wa Tanzania nchini Zambia umekuwa ofisi ya kwanza ya uwakilishi kutembelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax tangu aapishwe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kushika wadhifa huo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza na watumishi (hawapo pichani) wa Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania jijini Lusaka, Zambia katika kikao kilichofanyika katika Ofisi za Ubalozi huo tarehe 13 Oktoba 2022.
Mhe. Dkt, Tax (kulia) akiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine wakifuatilia kikao hicho kilichofanyika tarehe 13 Oktoba 2022 jijini Lusaka Zambia.
Mheshimiwa Waziri Tax akisaini kitabu cha wageni baada ya kuwasili katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Zambia tarehe 13 Oktoba 2022 jijini Lusaka Zambia, kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Zambia anayemaliza muda wake, Mhe. Hassan Simba Yahya.
Maafisa wa Ubalozi wakifuatilia kikao hicho.
Kutoka Kulia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakipokea taarifa ya maendeleo ya ukarabati wa jengo la ofisi na nyumba za Serikali ya Jamhuri ya Tanzania zilizopo nchini Zambia kutoka kwa Mhe. Balozi Hassan Yahya Simba alipotembelea nyumba za watumishi wa Ubalozi huo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akitoa maelekezo kwa Mkuu wa Utawala na Fedha wa Ubalozi huo Bw. Humphrey Shangarai (kushoto) alipotembelea nyumba za watumishi wa ubalozi huo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akisaini kitabu cha wageni baada ya kuwasili katika ofisi za Bandari ya Dar es Salaam (TPA) zilizopo jijini Lusaka, Zambia tarehe 13 Oktoba 2022. Aliyesimama ni Mwakilishi wa TPA nchini Zambia, Bw. Hamis Chambali.
Picha ya pamoja.
0 Comments