Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (katikati) akikagua kazi ya ujenzi iliyofanyika kwenye mradi wa ujenzi wa mnada wa Malampaka uliopo Wilayani Maswa Mkoani Simiyu. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Aswege Kaminyoge na kulia ni Mkurugenzi wa idara ya Uzalishaji na Masoko, Bw. Stephen Michael.
Mkurugenzi wa idara ya Uzalishaji na Masoko, Bw. Stephen Michael (kulia) akifafanua jambo kuhusu mradi wa ujenzi wa mnada wa Malampaka uliopo Wilayani Maswa Mkoani Simiyu kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki mara baada ya Waziri Ndaki kukagua mradi huo ambapo aliagiza kusitishwa kwa mkataba wa ujenzi kutokana na kutoridhishwa na kazi iliyofanyika kulingana na mkataba.
..............................
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayesimamia Sekta ya Mifugo kusitisha mkataba wa ujenzi wa Mnada wa Malampaka unaojengwa na Kampuni ya Kumuli Engineering and Liveline Technology.
Waziri Ndaki ametoa agizo hilo leo (01.10.2022) baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mnada huo uliopo katika Kata ya Malampaka Wilayani ya Maswa Mkoani Simiyu ambapo hakuridhishwa na kazi iliyofanywa na mkandarasi huyo.
Mkandarasi huyo alipewa kazi ya ujenzi wa mnada huo Januari 25, 2022 na alitakiwa kumaliza ujenzi Mei 23, 2022. Kutokana na kushindwa kumaliza kazi kwa muda aliongezewa muda mpaka Agosti 8, 2022. Lakini mpaka Waziri Ndaki alipofika kukagua kazi iliyofanyika ilikuwa ni asilimia 9.2.
Kutokana na hali hiyo, Waziri Ndaki amemuagiza Katibu Mkuu anayesimamia Sekta ya Mifugo kusitisha mkataba wa ujenzi wa mnada na Kampuni ya Kumuli Engineering and Liveline Technology. Pili alimuagiza Kamanda wa Polisi Wilaya ya Maswa kumtafuta mmiliki wa kampuni hiyo ili arudi kulipa madeni ya wafanyakazi wake pamoja na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Aidha, amemuagiza Katibu Mkuu anayesimamia Sekta ya Mifugo kuhakikisha anamtafuta mkandarasi mwingine haraka ili ujenzi wa mnada huo uweze kukamilishwa na kuanza kutumika. Lakini pia alisema kuwa kama hatua za kumpata mkandarasi mwingine zitachukua mud ani vema ujenzi huo ukafanyika kwa kutumia wataalam wa ndani ili mnada uanze kufanya kazi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Aswege Kaminyoge amesema kuwa mkandarasi huyu ameshapewa muda wa kutosha lakini bado kazi halakamilisha, lakini pia ameondoka bila kuwalipa wafanyakazi pamoja na watoa huduma hivyo ni vyema akawalipa wafanyakazi wake.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi, Wambura Richard amesema kuwa jumla ya deni wanalodai ni shilingi 9,544,300 hivyo ameiomba serikali kuwasaidia ili waweze kulipwa fedha hizo.
Ujenzi wa Mradi huo wa Mnada wa Malampaka unagharimu shilingi milioni 261 na mkandarasi alikuwa ameshalipwa shilingi milioni 44 ambayo kazi yake ilitakiwa ifikie asilimia 17 lakini licha ya kuchelewa bado kazi ipo asilimia 9.2.
0 Comments