**************
Na. WAF - Dar es Salaam
Katibu Mkuu, Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi amesaini makubaliano ya kiasi cha Shilingi Bil 98.2 na nchi zinazochangia Mfuko wa Afya wa pamoja Health Basket Fund (HBF) inayojumuisha nchi za Denmark, Canada, Ireland, South Corea, Swaziland, UNFPA na UNICEF kwa kwa lengo la kusaidia huduma za Sekta ya Afya nchini.
Makubaliano hayo yamefanyika leo Octoba 27, 2022 jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka wizara ya Afya, Wizara ya Fedha na Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Prof. Makubi amesema Makubaliano hayo ya kusaini fedha hizo yametokana na juhudi za Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha tunaboresha mashirikiano na nchi zetu marafiki.
"Fedha hizi zitaenda kutumika kwenye mwaka wa fedha 2022/2023 na asilimia 90 ya fedha zinaenda kuimarisha huduma katika ngazi ya Afya msingi kuanzia ngazi ya Wilaya, Vituo vyote vya Halmashauri, Vituo vya kati na Zahanati kwa kununua Dawa, pamoja na vipimo."Amesema Prof. Makubi
Akifafanua Asilimia 10 inayobaki Prof. Makubi amesema inagawanywa katika makundi mbalimbali ya kusimamia ambapo 2% inakwenda TAMISEMI, 4% inakwenda Wizara ya Fedha na Mipango na 4% inaenda kwenye Ofisi ya Mkaguzi Wa Serikali kwa lengo la kukagua fedha hizo zinatumika kwa lengo lililowekwa.
"Lengo la Serikali yetu ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za Afya hivyo tunawakaribisha Wadau wengine waweze kuchangia mfuko huu kwa kuongezea pale ambapo Serikali imeweka bajeti yake." Amesema Prof. Makubi
Mwisho, Prof. Makubi amefanunua kuwa Serikali inatenga bajeti yake kuwasaidia wananchi japo wanapotokea wadau kuchangia maendeleo ya Tanzania wanakaribishwa ili nguvu iongezeke katika mfuko wa (HBF).
0 Comments