Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YASISITIZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KATIKA ULINZI NA UFUATILIAJI MIENENDO YA WANYAMAPORI


Serikali Kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imesema itaendelea kutumia teknolojia ya kufuatilia mienendo ya wanyamapori katika maeneo ya hifadhi kwa kuwa imesaidia kwa kiasi kikubwa katika kutambua mienendo ya wanyamapori mbalimbali wakiwemo wale walio hatarini kutoweka na wanaosababisha migogoro kwenye jamii.

Kauli hiyo imetolewa leo mkoani Morogoro na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana alipokua akizindua zoezi la Kuvisha Mikanda yenye Redio za Mawasiliano kwa wanyamapori linalofanywa na Watalaam kutoka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania ( TAWIRI) lililofanyika katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi ambapo jumla ya makundi 53 ya wanyamapori yanatarajiwa kifungwa mikanda hiyo nchi nzima.

"Katika kufuatilia mienendo ya wanyamapori waliohatarini kutoweka, teknolojia hii husaidia kutambua uwepo wao, mienendo na mtawanyiko katika mifumo ikolojia yao. Utambuzi huu husaidia katika kuimarisha nyanda za malisho na ulinzi." amesema Balozi Dkt . Chana

Amesema kwa upande wa wanyamapori waharibifu, teknolojia hiyo husaidia kutambua makundi na mienendo yao na kutoa taarifa mapema kuhusu uwepo wa makundi hayo nje ya hifadhi na kichukua hatua kabla ya hayajasababisha madhara.

"Taarifa hizi husaidia katika kupanga mbinu muafaka za kukabiliana na wanyamapori hao. " amesisitiza Balozi Dkt. Chana

Katika hatua nyingine ameeleza kuwa zoezi hilo alilolizindulia limelenga kuimarisha uhifadhi na utalii kusini mwa Tanzania hususan katika Hifadhi za Taifa za Nyerere, Ruaha na Mikumi akifafanua kuwa litasaidia kwa kiwango kikubwa katika kupunguza migogoro baina ya jamii zinazozunguka hifadhi. "Jumla ya makundi ya wanyamapori 53 yatafungwa mikanda hii yenye redio za mawasiliano katika hifadhi hizi tatu." amesisitiza Balozi Dkt. Chana

Sambamba na hayo, Waziri Balozi Dkt. Pindi Chana ameongeza kuwa wanyamapori watakaofungwa mikanda hiyo ni pamoja na makundi ya tembo, simba, chui, duma, mbwa mwitu na twiga.

Aidha, taarifa na takwimu hizo zitasaidia kuandaa ramani za mitawanyiko ya wanyamapori katika misimu na nyakati mbalimbali ambazo zitasaidia kufungua njia mpya za utalii “tourism circuits” pamoja na kuimarisha uhifadhi wa wanyamapori katika hifadhi hizo.

Naye Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Prof. Eliamani Sedoyeka amesema Tekinolojia hiyo itasaidia kuwalinda Wanyamapori na Hifadhi zetu hapa nchini. Pia, itasaidia kufuatilia mienendo ya Wanyamapori hai na kuweza kuwaona kidijitali pindi wanapotaka kuleta madhara.

"Kwa kutumia tekinolojia hii tunaweza kuwaona kidijitali wanapotembea na hasa wanapokaribia maeneo hatarishi ya kuleta madhara kwa wananchi"

Post a Comment

0 Comments