Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Hamad Hassan Chande (Mb) akiwataka wataalamu wa maboresho makubwa ya Mfumo wa Ununuzi Serikalini, kuhakikisha wanamaliza kazi kwa wakati, alipofanya ziara ya kukagua mfumo huo, mkoani Iringa.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Bw. Eliakimu Maswi (kulia), akimuongoza Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Hamad Hassan Chande (Mb) alipowasili katika Chuo cha Mkwawa Mkoani Iringa, kukagua mfumo wa ununuzi wa umma, kushoto ni Naibu Rasi Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam wa Chuo cha Mkwawa, Prof. Deusdedit Rwehumbiza.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Hamad Hassan Chande (Mb) akisalimiana na Mbunge wa Iringa Mjini, Mhe. Jesca Msambatavangu, wakati wa ziara ya kukagua mfumo wa ununuzi wa umma, mkoani Iringa.
Mkurugenzi wa Mifumo na Mawasiliano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Bw. Michael Moshiro, akieleza changamoto katika Mfumo wa sasa Ununuzi wa Umma (TANePS), wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Hamad Hassan Chande (Mb) (kushoto) ya kukagua mfumo wa ununuzi wa umma, mkoani Iringa.
Baadhi ya wataalamu wa uboreshaji mkubwa wa Mfumo wa Ununuzi wa Umma, wakimsikiliza kwa makini Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Hamad Hassan Chande (Mb) (hayupo pichani), alipofanya ziara ya kukagua mfumo huo, mkoani Iringa.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Hamad Hassan Chande (Mb) (wa nne kushoto), Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) Bw. Eliakimu Maswi (wan ne kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na wataalamu wa maboresho ya Mfumo wa Ununuzi wa TANePS, mkoani Iringa.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WFM- Iringa)
***************************
Na. Peter Haule na Haika Mamuya, WFM, Iringa
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande, amesema kuwa Serikali imeweka udhibiti wa mianya ya rushwa na ubadhirifu wa fedha za umma uliosababishwa na kasoro katika Mfumo wa Ununuzi wa Umma (TANePS) kwa kufanya maboresho makubwa ya mfumo huo.
Hayo yamebainishwa mkoani Iringa wakati alipofanya ziara ya kukagua maboresho ya mfumo huo yanayofanywa na wataalamu wa ndani kwa lengo la kuondoa changamoto zilizopo na kukidhi mahitaji halisi ya Serikali na wazabuni.
Mhe. Chande alisema kuwa kumekuwa na changamoto ya kupata thamani halisi ya fedha katika huduma na bidhaa kutokana na mianya ya rushwa iliyokuwepo katika mfumo wa manunuzi ambayo inasababisha utofauti mkubwa wa gharama kwenye eneo moja.
“Kumekuwa na usiri mkubwa katika michakato ya ununuzi, hali inayofanya mtu ajiulize huu usiri una nini katikati yake, ununuzi unatakiwa ufanyike kwa uwazi na haki hivyo wataalamu mnaofanya maboresho haya mnaweza kututengenezea mfumo unao akisi uhalisia katika ununuzi na utakaosaidia manunuzi kuanyika kwa haki” alisema Mhe. Chande.
Alisema kuwa nia ya Serikali ya kufanya maboresho hayo ni kuhakikisha taasisi nunuzi zinatoka katika mazoea ya kufanya michakato ya ununuzi nje ya mfumo kwa kuwa ununuzi wa nje ya mfumo unaongeza uwezekano wa rushwa na upotevu wa thamani ya fedha.
Aidha Mhe. Chande alisema zipo faida nyingi ambazo Serikali itazipata baada ya maboresho hayo kukamilika ikiwemo kuimarika kwa uchumi wa nchi kwa kuokoa mapato ya Serikali yanayopotea kwa kuwa asilimia 70 ya matumizi yote ya bajeti ya nchi yameelekezwa katika ununuzi.
Pia alimtaka Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Bw. Eliakumu Maswi, kuhakikisha wote wanaotakiwa kutumia mfumo huo wamnautumia, kwa kuwa itasikitisha kuona wataalamu wanatumia muda na nguvu zao katika kufanya maboresho ya mfumo halafu wengine wanakaidi kuutumia.
Mhe. Chande ameipongeza PPRA kwa juhudi wanazoendelea nazo za kusimamia maboresho makubwa katika mfumo wa ununuzi ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi katika Sekta ya Ununuzi nchini
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Bw. Eliakumu Maswi, alimuahidi Mhe. Naibu Waziri huyo kuwa maboresho ya mfumo huo yatauwezesha kuwa bora katika nchi za Afrika Mashariki na kusini mwa Afrika.
Pia atahakikisha wote wanaotakiwa kuutumia mfumo huo wanasajiliwa ili lengo la kufanya kazi za ununuzi wa umma kwa uwazi linafikiwa na kuwa chachu ya maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Naye Mbunge wa jimbo la Iringa mjini, Mhe Jesca Msambatavangu, aliipongeza Serikali kwa kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kuhakikisha yanafanyika maboresho makubwa ya mfumo wa ununuzi wa umma kwa kuwa si jambo rahisi kuingia katika maboresho hayo bila kuwa na msaada kutoka kwa wataalam wa nje ya nchi.
Amewataka wananchi kuhakikisha wanatumia mfumo huo iwapo wanataka kufanya biashara na Serikali kwa kuwa utakuwa rahisi kuutumia na umeangalia hali halisi ya mtanzania na soko la ndani.
Uamuzi wa maboresho ya Mfumo wa Ununuzi nchini ulitokana na agizo la Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba, wakati wa uwasilishaji wa bajeti ya mwaka 2022/23 bungeni. Maboresho hayo yaliyoanza mwezi julai 2022 yanatarajia kufanyika kwa awamu sita ambapo mpaka sasa awamu ya kwanza tayari imekwisha kamilika na inatarajiwa majaribio yake yaanze mwezi Desemba 2022.
0 Comments