Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI KUFANYA MABORESHO MAKUBWA KATIKA MIFUMO YA UNUNUZI.


Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Hamad Hassan Chande (Mb) akiwataka wataalamu wa maboresho makubwa ya Mfumo wa Ununuzi Serikalini, kuhakikisha wanamaliza kazi kwa wakati, alipofanya ziara ya kukagua mfumo huo, mkoani Iringa.


Mkurugenzi wa Mifumo na Mawasiliano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Bw. Michael Moshiro, akieleza changamoto katika Mfumo wa sasa Ununuzi wa Umma (TANePS), wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Hamad Hassan Chande (Mb) (kushoto) ya kukagua mfumo wa ununuzi wa umma, mkoani Iringa.
Baadhi ya wataalamu wa uboreshaji mkubwa wa Mfumo wa Ununuzi wa Umma, wakimsikiliza kwa makini Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Hamad Hassan Chande (Mb) (hayupo pichani), alipofanya ziara ya kukagua mfumo huo, mkoani Iringa.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Hamad Hassan Chande (Mb) (wa nne kushoto), Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) Bw. Eliakimu Maswi (wan ne kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na wataalamu wa maboresho ya Mfumo wa Ununuzi wa TANePS, mkoani Iringa.

(Picha na Kitengo cha Uhusiano kwa Umma-PPRA)



*******************

Na Zawadi Msalla-Iringa

Naibu Waziri, wa Fedha na Mipango Mhe. Hamad Hassan Chande ameipongeza PPRA kwa juhudi wanazoendelea nazo za maboresho makubwa katika mfumo wa ununuzi wa kielektroniki. Maboresho hayo yaliyolenga kuongeza ufanisi wa utendaji kazi katika Sekta ya Ununuzi nchini yanafanyika kwa kutumia wataalam wa ndani ya nchi wa ujenzi wa mifumo ya TEHAMA . Akizungumza baada ya kutembelea kambi ya wataalam hao mkoani Iringa katika Chuo kishiriki cha Elimu Mkwawa Mhe. Chande alisema ni imani yake kuwa maboresho hayo yatasaidia taasisi nunuzi kuweza kufanya michakato ya ununuzi kwa uwazi na ubora unaotakiwa.

Mhe. Chande aliongeza kuwa zipo faida nyingi ambazo Serikali itazipata baada ya maboresho haya kukamilika ikiwemo kuondoa changamoto ambazo zipo katika mfumo wa sasa wa TANePS. Watu wengi wamekuwa wakilalamika kuwa mfumo huu si rafiki kwa watumiaji. Hivyo basi katika kuhakikisha changamoto hii inatatuliwa wataalamu wapo kazini kuona mfumo huu uweze kufanya kazi mpaka kwa kutumia vishikwambi, alieleza.

“Kama watu hawafundishwi jinsi ya kutumia mitandao ya kijamii lakini wanaweza kutumia, hata mfumo huu itakuwa rahisi kutumia kwa kila mtu” alisema Mhe. Naibu Waziri

Akiongea na wataalam wa mifumo alisema ni lazima wafahamu nia ya Serikali ya kuamua kufanya maboresho hayo kuwa ni kuhakikisha taasisi nunuzi zinatoka katika mazoea ya kufanya michakato ya ununuzi nje ya mfumo kwani ununuzi wa nje ya mfumo unaongeza uwezekano wa rushwa na upotevu wa thamani ya fedha.

“Kumekuwa na usiri mkubwa katika michakato ya ununuzi, hali inayofanya mtu uwaze huu usiri una nini katikati yake, ununuzi unatakiwa ufanyike kwa uwazi na haki, ni nyie mliopo hapa mnayofanya haya maboresho mnaweza kututengenezea mfumo unao akisi uwazi katika ununuzi na utakaosaidia manunuzi yoyote yanayofanyika kuwa ya haki” alisema.

Mfumo huu kama utatumiwa ipasavyo uchumi wa nchi utaenda kuimarika, kwani asilimia 70 ya matumizi yote ya bajeti ya nchi umejikita katika ununuzi. Maboresho haya yataweza kuleta upatikanaji wa thamani ya fedha kwani kama mchakato wote utafanyika ndani ya mfumo utaondoa mianya ya rushwa katika ununuzi.

Hatahivyo alimtaka mtendaji Mkuu wa PPRA, Eliakumu Maswi kujipanga na kuangalia jinsi ya kuweza kuutunza mfumo huo ulioboreshwa ilikuhakikisha unakuwa na unatenda kazi unaoimarika kila siku. Alisema itasikitisha kuona wataalamu wametumia muda na nguvu zao kwa kiwango cha juu na baada ya hapo mfumo ushindwe kutunzwa.

Naye Mbunge wa jimbola Iringa mjini , Mhe Jesca Msambatavangu aliipongeza Serikali kwa kupitia Wizara ya Fedha na Mipango na kwa kushirikiana na PPRA umeufanya, alisema si jambo rahisi kuingia katika maboresho makubwa kama yanavyoendelea sasa bila kuwa na msaada kutoka kwa wataalam wa nje ya nchi.

Alisema Faraja yake ni kuwa wataalamu waliofanya maboresho haya ni wazawa ni imani yake kuwa mfumo utakuwa umeangalia hali halisi ya mtanzania na soko la ndani. Alisema mafanikio ya maboresho haya yametokana na wataalam wazawa kujiamini kuwa inawezekana bila wataalam kutoka nje ya nchi.

Aliwakumbusha wataalam hao kuwa uzalendo waliouonesha wakati wakiendelea na maboresho ya mfumo utakumbukwa kwa vizazi vyao vyote. Hata hivyo aliwataka uzalendo waliouonesha usiishie wakati wa huu, hata baada ya kumaliza kazi hii ni vema wakumbuke bado Taifa linawahitaji. Moyo wa uzalendo uwe mbele zaidi katika kulitoa Taifa katika umaskini na kulifanya liwe ni moja ya taifa linalotegemewa.

Uamuzi wa maboresho ya Mfumo wa Ununuzi nchini ulitokana na agizo la Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Mwigulu Nchemba wakati wa uwasilishaji wa bajeti ya mwaka 2022/23 bungeni. Maboresho hayo yaliyoanza mwezi julai 2022 yanatarajia kufanyika kwa awamu sita ambapo mpaka sasa awamu ya kwanza tayari imekwisha kamilika na inatarajiwa majaribio yake yaanze mwezi desemba 2022.






Post a Comment

0 Comments