*************************
Na Mwandishi Wetu
MAOMBI maalum ya kuwaombea viongozi wakuu wa nchi,pamoja na Tanzania kwa ujumla yanatarajia kuanza leo (jumatatu)jijini Dar es Salaam.
Maombi hayo ya wiki moja yatakayoambatana na semina ya neno la Mungu yameandaliwa na kanisa la Calvary Tanzania Assemblies of God (CAG) 'Chuo cha Manabii',lililopo eneo la Bandari Kavu, Ubungo Maziwa.
Akizungumza kanisani hapo jana,Katibu wa Kanisa hilo Lucas John alisema maombi hayo ni sehemu ya kutimiza maandiko katika biblia.
"Maandiko katika waraka wa kwanza kwa Timotheo 2:1-2,Mungu ameliagiza kanisa kufanya maombi kwa ajili ya viongozi na wenye mamlaka ili Taifa lidumishe upendo,amani na utulivu,"alisema
"Kufanya hivi ni katika kutii agizo hilo pamoja na kutekeleza moja ya majukumu ya msingi ya kanisa letu,"aliongeza
Katibu huyo alisema maombi hayo yataongozwa na Mchungaji Kiongozi wa Kanisa hilo,Imelda Maboya akishirikiana na viongozi wengine,yatafikia tamati jumapili ijayo Octoba 16,2022
"Tunawakaribisha watu kutoka sehemu mbalimbali jijini kuhudhuria maombi haya yatakayokuwa yakianzaa saa 11 jioni kanisani hapa,"aliongeza.
CAG ina makanisa zaidi ya 1500 Tanzania Bara na Zanzibar.
0 Comments