Ticker

6/recent/ticker-posts

DKT. STERGOMENA TAX APOKEA UJUMBE MAALUM KUTOKA MISRI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax amepokea ujumbe maalum kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Mhe. Sameh Hassan Shoukry uliowasilishwa kwake na Mjumbe Maalum ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayeshughulikia masuala ya Afrika wa nchi hiyo, Mhe. Sherif Issa.

Akizungumza mara baada ya kupokea ujumbe huo leo tarehe 26 Oktoba 2022 jijini Dar es Salaam, Mhe. Dkt. Tax ameishukuru Serikali ya Misri kwa kuendelea kuthamini ushirikiano wa kihistoria uliopo baina yake na Tanzania hususan kwenye sekta ambazo zinagusa maisha ya wananchi moja kwa moja kama afya, elimu, maji, nishati na ujenzi wa miundombinu.

Amesema, ni kutokana na kuthamini mchango unaotolewa na Misri kwenye sekta mbalimbali za maendeleo nchini Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alifanya ziara nchini humo mwezi Novemba 2021 na maeneo mbalimbali ya ushirikiano yalijadiliwa na kukubalika.

“Ninayo furaha kukukaribisha nchini Mhe. Waziri. Nakiri kupokea ujumbe huu muhimu kutoka kwa Waziri mwenzangu. Nitaupitia na kuufanyia kazi na kuwasilisha kwenu mrejesho haraka iwezekanavyo”, amesema Mhe. Dkt. Tax.

Naye, Mhe. Issa amempongeza Mhe. Dkt. Tax kwa kuteuliwa katika wadhifa huo mpya na kumweleza utayari wa Serikali ya Misri katika kushirikiana naye.

Kadhalika amesema, Serikali ya Misri itaendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutekeleza na kukamilisha miradi yote ya pamoja ambayo nchi hizo zimekubaliana ukiwemo Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere.

“Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere ni kwa ajili ya Watanzania. Mradi huu ni mkubwa na wa kwanza kwa Misri kuutekekeleza hapa nchini. Hivyo tutajitahidi kama Serikali kushirikiana na Tanzania ili kuhakikisha mradi wote unakamilika na kukabidhiwa”, alisisitiza Mhe. Issa.

Pia Mhe. Issa alitumia nafasi hiyo kuikaribisha Tanzania kushirki kwenye Mkutano wa 27 wa Kimataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP27) utakaofanyika mwezi Novemba 2022 katika Mji wa Sharm El Sheikh, nchini humo.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba ambaye alishiriki mazungumzo hayo amesema, Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme wa Julius Nyerere ni alama ya ushirkiano kati ya Tanzania na Misri na kwamba Wizara yake itaendelea kutoa ushirikiano wote unaohitajika kwa Serikali ya Misri na Timu ya Wataalam wa Mradi huo ili kuufanikisha.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akipokea ujumbe maalum kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Mhe. Sameh Hassan Shoukry uliowasilishwa kwake na Mjumbe Maalum ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri anayeshughulikia masuala ya Afrika wa nchi hiyo, Mhe. Sherif Issa.Mhe. Dkt. Tax amepokea ujumbe huo leo tarehe 26 Oktoba, 2022 akiwa katika Ofisi Ndogo za Wizara zilizopo jijini Dar es Salaam
Mhe. Dkt. Tax akiwa katika mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri anayeshughulikia masuala ya Afrika, Mhe. Sherif Issa
Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba ambaye alishiriki mazungumzo hayo naye akichangia jambo
Mazungumzo yakiendelea
Mhe. Dkt. Tax na mgeni wake wakimsikiliza Balozi wa Misri hapa nchini Mhe. Mohammed Gaber Abulwafa wakati akifafanua jambo
Mhe. Makamba akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Bw. Maharage Chande pamoja na wadau wengine wakaishiriki mazungumzo kati ya Mhe. Dkt. Tax na Mhe. Issa (hawapo pichani)
Picha ya pamoja

Post a Comment

0 Comments