Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt.Allan Kijazi akizungumza na waanidhsi wa habari leo Septemba 2,2022 Jijini Dar es Salaam.
********************
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt.Allan Kijazi amesema kupitia kamati aliyoiunda ya kutatua migogoro ya Ardhi Jijini Dar es Salaam imebaini vyanzo vikuu nane vya migogoro ikiwemo uvamizi,kughushi nyaraka na utapeli.
Dkt. kijazi ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya matokeo ya ripoti iliyowasilishwa kwake na kamati ya wataalamu, ambapo amesema Mnamo tarehe 25 Julai, 2022 aliunda Kamati ya Wataalam wa Wizara na Mkoa wa Dar es Salaam kwa ajili ya kupokea na kusikiliza malalamiko ya wananchi kwa lengo la kuyapatia ufumbuzi.
Ameongeza kuwa vyanzo vya migogoro vilivyobainishwa ni pamoja na uwepo wa milki pandikizi za ardhi ambapo hoja 13 ziliibuliwa sawa na asilimia 3.3%,uvamizi wa maeneo yenye milki za watu wengine ambapo hoja 99 ziliibuliwa sawa na asilimia 25% ,kughushi nyaraka ambapo hoja 16 ziliibuliwa sawa na asilimia 4.1% madai ya fidia ambapo hoja 62 ziliibuliwa sawa na asilimia 15.9%,uelewa mdogo wa taratibu za ardhi na masuala ya mikataba ambapo hoja 95 ziliibuliwa sawa na asilimia 24.3%.
Aidha,Dkt.Allan ameyataja masuala ya mirathi kuchangia migogoro ya Ardhi ambapo hoja 12 ziliibuliwa sawa na asilimia 3.1% migogoro iliyotolewa uamuzi na mahakama au mamlaka nyinyinge ambapo hoja 65 ziliibuliwa sawa na asilimia 16.6 na changamoto za urasimishaji ambapo hoja 29 ziliibuliwa sawa na asilimia 7.4%
"Kamati hiyo ilijumuisha wataalamu kutoka vyombo vya ulinzi na usalama ili kuongeza uwazi na ufanisi katika zoezi hili,napenda kuwataarifu kuwa kamati ilianza kutekeleza zoezi hilo kuanzia agosti mosi 2022 hadi tarehe 5 Agosti, 2022"
"Kamati hiyo imekamilisha uchambuzi wa masuala muhimu yaliyojitokeza na inaendelea kuratibu na kusimamia utekeleza wake hasa kwa masuala ambayo vikao vya usuluhishi, uhakiki wa uwandani, ufufuaji wa mipaka, madai ya fidia, upangaji na umilikishaji" Alisema Dkt.Kijazi.
Ameongeza kuwa, Kamati ilipokea malalamiko 391 kutoka kwa wananchi wa halmashauri zote tano za Mkoa wa Dar es Salaam na hoja tatu kutoka Mkoa wa Pwani katika Wilaya za Kibaha na Kisarawe.
Amesema Halmashauri ya Manispaa ya Temeke imetoa jumla ya hoja na malalamiko 41 yaliibuliwa, Kinondoni ni 144, Kigamboni ni 39, Ubungo ni 86, na ilala 78 ambapo kamati iliwasikiliza wananchi na kupokea nyaraka ambazo zilisaidia kufikia uamuzi.Miongoni mwa kazi zilizofanyika ni ukaguzi wa maeneo 36 kati ya 38 yenye changamato za uvamizi, upimaji na kubainisha mipaka.
"Wananchi 191 wamepewa majibu na hatua zinazopaswa kuchukuliwa kuhusu malalamiko yao na wapo wananchi ambao wameonyesha kutorizishwa na hatua zilizochukuliwa niwaambie tu wizara itaendelea kuwasikiliza na kufikia maamuzi ambayo yataleta matokeo chanya na nisisitize tu zoezi hili niendelevu" Alisema Kijazi.
Aidha, amesema masuala yaliyobakia ni uhakiki wa maeneo, ufufuaji na urejeshaji wa mipaka, uchambuzi wa madai ya fidia na viwanja mbadala, changamoto zinazotokana na urasimishaji, ukamilishaji wa umilikishaji ardhi, vikao vya usuluhishi ambapo yataendelea kufanyiwa kazi hadi ifikapo Septemba 20, Mwaka huu.
Aidha Baada ya kuhitimisha zoezi hili katika Mkoa wa Dar es Salaam, zoezi kama hilo litafanyika kwenye Mkoa wa Dodoma na kufwatiwa na mikoa mingine kulingana na ratiba itakayotolewa.
0 Comments