Mkuu wa wilaya ya Kishapu Joseph Mkude Shinyanga akizungumza katika maadhimisho ya siku ya wazee duniani mkoa wa Shinyanga kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Dkt. Sophia Mjema
Mtaalamu Dominick akiendelea kutoa elimu ya afya juu ya ugonjwa wa Ebola na kuhamasisha wazee na wananchi kuchanja chanjo ya UVIKO -19
Wazee wakimsikiliza mkuu wa wilaya ya Kishapu.
Wazee wakiwa katika maadhimisho hayo.
Wazee wakifuatilia kilichokuwa kinaendelea
Wazee wakifuatilia kilichokuwa kinaendelea
***
Kila tarehe Moja ya Mwezi Oktoba (Oktoba Mosi) ni siku ambayo dunia nzima huadhimisha siku ya Wazee kwa lengo la kuwatambua na kuwaenzi wazee.
Mkoa wa Shinyanga umeadhimisha siku hii muhimu Septemba 27,2022 katika kata ya Mwamalasa wilayani Kishapu mkoani Shinyanga ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa wilaya ya Kishapu Joseph Mkude kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Dkt. Sophia Mjema.
Akihutubia katika maadhimisho hayo, Mkude alisema serikali inatambua umri wa mzee ni kuanzia miaka 60 na kuendelea na kwamba kila mmoja anapaswa kutambua kuwa siku moja ataufikia uzee hivyo wazee wanapaswa waheshimiwe,watunzwe na kuenziwa.
“Nawasihi tutumie hekima na ushauri walionao wazee wetu na siyo kuanza kuwafanyia vitendo vya ukatili kwa kuwanyanyasa,kuwatenga na kuwaua kwa imani potofu,na serikali itaendelea kuchukua hatua kali za kisheria kwa watakaonyanyasa wazee kwa namna yoyote ile”,alisema Mkude.
Katika hatua nyingine aliziagiza halmashauri za wilaya mkoani Shinyanga ambazo hazijatekeleza zoezi la kutambua wazee na kuwapatia kadi za matibabu bila malipo kuhakikisha wanatekeleza agizo hilo pamoja na kutenga madirisha ya wazee katika vituo vya afya na Zahanati.
Aidha aliwahakikishia wazee kuwa mkoa wa Shinyanga utaendelea kuhakikisha kuwa dawa zote za magonjwa ya wazee zinapatika kwenye vituo afya huku akiwataka wakurugenzi wa halmashauri kufanya ukaguzi wa dawa na kuwashirikisha wazee katika shughuli zao.
Alitoa rai kwa uongozi wa idara za afya kuanzia ngazi ya mkoa kuhakikisha kuwa uwepo wa vyumba maalum vya kutolea huduma za afya kwa wazee na kuwapa kipaumbele na kuweka ujumbe wa “Mpishe Mzee Apate Huduma Kwanza”.
Akisoma risala, katibu msaidizi wa Baraza la Wazee mkoa wa Shinyanga,Suzana Masebu aliomba changomoto zinazowakumba wazee zishughulikiwe ili wazee waishi kwa amani na usalama.
“Tunaishukuru serikali kwa kuendelea kuheshimu na kutambua mchango wa wazee kwa kukemea vitendo vya unyanya saji na kuchukua hatua kwa wanaokiuka haki za binadamu huku wakiomba elimu iendelee kutolewa kwa jamii kuhusu sera ya taifa ya wazee,haki na wajibu wa kuwalinda wazee”,alisema Suzana.
Maadhimisho ya siku ya wazee duniani mkoa wa Shinyanga yameenda sambamba na zoezi la kucheza michezo mbalimbali ikiwemo kuvuta kamba na kufukuza kuku ambapo washindi wamejinyakulia zawadi mbalimbali katika maadhimisho hayo.
Pia kumefanyika zoezi la upimaji afya kwa wazee wote pamoja na wananchi wengine ambapo washiriki wa maadhimisho hayo wamepima bure magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari,shinikizo la damu,magonjwa ya macho na mengineyo ikiwa nisambamba na kutoa elimu ya Ugonjwa wa Ebola na Kuhamasisha wazee kuendelea kuchanja chanjo ya UVIKO -19.
0 Comments